MTANGAZAJI

ATHARI ZA KUFUNGWA KWA SERIKALI MAREKANI

 


Marekani inaendelea kukumbwa  na athari za kufungwa kwa serikali ya shirikisho, hatua iliyoathiri zaidi ya wafanyakazi milioni 1.4 wa serikali. Kati ya hao, takribani 670,000 walibaki nyumbani bila malipo, huku wengine 730,000 wakifanya kazi muhimu kama usalama wa viwanja vya ndege na ulinzi wa mipaka bila kupokea mshahara. Hali imezua tatizo la kifedha, hususani kwa familia zinazotegemea mshahara wa juma kwa matumizi ya kila siku.

 Serikali ya shirikisho ya Marekani ilianza kufungwa rasmi Oktoba mosi 2025 , baada ya mchakato wa kifedha wa serikali kuisha bila bajeti mpya au kuongezewa muda.

Katika sekta ya huduma kwa jamii, mpango wa chakula kwa watu wenye kipato cha chini SNAP umeathirika pakubwa. Kwa mfano,jimbo la Georgia limeeleza kuwa zaidi ya familia 200,000 zilichelewa kupokea mgao wao wa mwezi. Hii imeongeza shinikizo kwa hifadhi za chakula na mashirika ya misaada.

Athari zimeonekana pia katika usafiri wa ndege za ndani na nje ya Marekani. Kutokana na upungufu wa watendaji wa udhibiti wa waongozaji wa ndege kwenye viwanja, zaidi ya safari 1,500 zimechelewa au kufutwa ndani ya majuma mawili ya mwanzo. Mfano mmoja ni uwanja wa ndege wa Denver, ambako siku moja ilishuhudia safari 115 zikifutwa kwa siku moja idadi isiyo ya kawaida kwa kipindi cha kawaida cha mwaka nchini Marekani.

Kwenye upande wa uchumi, Ofisi ya Bajeti ya Kongresi inakadiria kuwa Marekani inaweza kupoteza kati ya dola bilioni 7 hadi 14 ikiwa ufungwaji wa serikal ungeendelea kwa muda mrefu. Hadi sasa, ukuaji wa uchumi katika robo ya mwisho ya mwaka umeshuka kwa takribani asilimia 1.3, kutokana na kushuka kwa matumizi ya serikali na kuongezeka kwa usumbufu wa biashara.

Mashirika ya usalama wa taifa pia yameathirika. Kwa mfano, kikosi kinachosimamia silaha za nyuklia kimepunguza zaidi ya asilimia 80 ya wafanyakazi wake, hali inayoongeza shaka juu ya usimamizi wa shughuli za ulinzi.

Serikali ya Marekani iliendelea kukabiliwa na shinikizo kutoka kwa wananchi na wabunge kurejesha huduma za kawaida ili kuzuia madhara zaidi kwa uchumi, usafiri, na kaya za kipato cha chini.Baada ya siku 43 za kufungwa kwa serikali, Rais Donald Trump wa Marekani ametia saini ya sheria ya kufungua serikali tena usiku wa 12 Novemba 2025 baada ya kurejea kwa mkataba wa fedha ulopitishwa na bunge.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.