MTANGAZAJI

ECD YAONGOZA KWA WAUMINI WAADVENTISTA LICHA YA CHANGAMOTO

 


Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati katika kanisa la Waadventista wa Sabato  (ECD) inaendelea kuongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya waumini, ikiwa na idadi ya waumini  5,704,665. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa ripoti rasmi ya Taarifa ya Mwaka 2024 kutoka Ofisi ya Takwimu na Utafiti ya Kanisa hilo (ASTRA).

Divisheni zingine miongoni mwa 13 za kanisa hilo zenye idadi kubwa ya waumini ni Divisheni ya Afrika ya Kusini na Bahari ya Hindi (SID)- 4,334, 356,  Divisheni ya Amerika ya Kusini (SAD) - 2,704,791,  Divisheni ya Asia ya Kusini-Mashariki na Pasifiki (SSD) - 1,619,124, Divisheni ya Amerika ya Kaskazini (NAD) - 1,287,739,  Divisheni ya Asia ya Kusini (SUD) - 1,179,867, na Divisheni ya Afrika Magharibi na Kati (WAD) - 1,038,377.

 Divisheni za Ulaya na Mashariki ya Kati zina waumini wachache zaidi, hali inayoashiria changamoto za uinjilisti katika maeneo yenye kanuni kali za kijamii au kisheria.

Kanisa la Waadventista wa Sabato hadi mwishoni mwa mwaka 2024 lilikuwa na  jumla ya waumini  walioandikishwa wapatao milioni 23.68. 

Takwimu hizo zinaonesha kuwa ECD ambayo inajumuisha eneo la nchi 11 hadi mwaka 2024 ilikuwa na idadi ya makanisa mahalia ya Waadventista wa Sabato yapatayo 21,274 kutoka makanisa 13,423 yaliyokuwepo mwaka 2014, ambapo Kenya inaongoza katika eneo hilo kwa kuwa na makanisa 8,246 yenye waumini 1,327,638 ikifuatiwa na Tanzania yenye makanisa 4,898 yakiwa na waumini 1,146,727, na Rwanda inashika nafasi ya tatu ikiwa na makanisa 1,968 na waumini 1,186,613.

Kenya na Tanzania katika eneo hilo zimegawanywa kwenye maeneo mawili ya kiuongozi ya kanisa  ambapo Kenya kuna Unioni Konferensi mbili na Tanzania kuna Unioni Konferensi moja na Unioni Misheni moja.Takwimu za mwaka 2023 zinaonesha kuwa ECD ilichangia sehemu kubwa ya jumla ya watu zaidi ya milioni 1.4 waliobatizwa katika kanisa la Waadventista wa Sabato.

 Ongezeko hili la waumini katika eneo hilo linaelezwa ni kutokana na eneo hili linalojumuisha nchi zenye ongezeko kubwa la watu ikiwemo Tanzania, Kenya,Uganda na Ethiopia hali inayochangia fursa nyingi za utume. Pili, watu wa Afrika Mashariki na Kati wako tayari kupokea injili, tofauti na nchi za Magharibi ambako usasa umeenea.

ECD pia imeimarika kwa kuwa na uongozi ambao umekuwa mbele katika  mafunzo ya kina kwa wachungaji. Aidha, kampeni za uinjilisti wa kimataifa kwa kushirikiana na Vyombo vya Habari vya kanisa hilo Hope Channel, redio za AWR, huduma za vijana, wanawake na wanaume zimekuwa zikiwaleta wengi kwa Kristo. Washiriki wa kawaida nao wanahamasishwa kushiriki katika huduma za utume, huku taasisi za elimu na afya zikitoa huduma kwa jamii, na matukio ya matendo ya huruma kuwa lengo la utume .

Ripoti zinaonesha kuwa licha ya Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati (ECD) kuongoza kwa idadi ya waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato duniani, inakabiliwa na changamoto kadhaa. Kwanza ni udumishaji wa waumini, ambapo takribani 40 kati ya 100 waliobatizwa huacha kushiriki baada ya muda mfupi. Pili, ukosefu wa rasilimali ikiwemo majengo bora ya makanisa, vifaa vya kufundishia, na vyombo vya mawasiliano huathiri huduma.

Changamoto za kiuchumi kwa baadhi ya  waumini pia hupunguza ushiriki na utoaji, huku baadhi ya waumini wapya wakikosa mafundisho ya kina baada ya ubatizo. Vijana wengi wanakabiliwa na changamoto za kisasa, wakihisi kanisa halitoshelezi mahitaji yao. Baadhi ya maeneo yanakumbwa na uongozi dhaifu usio na mafunzo endelevu, migogoro ya ndani, na usimamizi duni wa baadhi ya miradi.


 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.