MTANGAZAJI

TUHUMA ZA UNYANYASAJI KINGONO WATIKISA DAYOSISI

 


Takriban theluthi moja kati ya Dayosisi 12 za Kikatoliki huko California,Marekani zimewasilisha kesi ya kufilisika au zinafikiria kufanya hivyo ili kushughulikia wimbi la kesi zilizowasilishwa na manusura wa unyanyasaji wa kingono utotoni baada ya sheria ya serikali kufungua dirisha la miaka mitatu ambapo kesi zilifunguliwa. 

Zaidi ya mashtaka 3,000 yamewasilishwa dhidi ya Kanisa Katoliki huko California chini ya sheria ya serikali ya 2019 ambayo iliruhusu waathiriwa kushtaki hadi umri wa miaka 40.

Mawakili wameshangazwa na idadi ya kesi zilizoibuka wakati wa muda huo wa miaka mitatu, ambalo lilifungwa mwishoni mwa Desemba.

Dayosisi ya Santa Rosa, ambayo inakabiliwa na kesi zaidi ya 200, iliwasilisha kesi ya kufilisika katikati ya Machi.Katika ombi lake la kufilisika, ilidai mali zenye thamani ya kati ya $10 milioni na $50 milioni. 

Dayosisi ya Oakland, inayokabiliana na takriban kesi 330 za unyanyasaji wa kijinsia, iliwasilisha kesi ya kufilisika mapema Mei. Ilidai mali yenye thamani ya kati ya $100 milioni na $500 milioni na makadirio ya madeni katika kiwango hicho hicho cha dola kwa mujibu wa  na ombi lake la kufilisika.

Askofu wa Oakland Michael C. Barber, katika barua, alisema, "maeneo ya ibada" yatafungwa, na Dayosisi italazimika "kufikiria upya" jinsi maeneo mengine yatakavyotumiwa.

Dayosisi ya San Diego ilifanya uamuzi mapema mwezi Mei mwaka huu wa kuwasilisha kufilisika wakati wa msimu huu wa kiangazi, anaeleza  Kevin Eckery, msemaji wa Dayosisi hiyo.

Kardinali Robert McElroy, Askofu wa Dayosisi ya San Diego, alitangaza mapema Februari mwaka huu uwezekano wa kufilisika huku Dayosisi hiyo ikikabiliwa na gharama za kisheria akizieleza kuwa za "kushangaza" katika kushughulikia kesi 400 zinazodai mapadri na wengine kunyanyaswa kingono.

Mengi ya madai ya unyanyasaji yaliyotajwa yalifanyika miaka 50 hadi 75 iliyopita, na madai ya awali yalianzia 1945.

Mali nyingi za Dayosisi hiyo, McElroy alisema katika barua, zilitumika kusuluhisha madai ya hapo awali, na kuishia na malipo ya dola milioni 198 mwaka 2007. Eckery ametabiri gharama ya kutatua kesi ambazo hazijakamilika dhidi ya dayosisi inaweza kufikia dola za kimarekani  milioni 550.




No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.