MTANGAZAJI

ALIYEWAHI KUWA KIONGOZI WA WAADVENTISTA ULIMWENGUNI AFARIKI

 


Benjamin D. Schoun, aliyewahi kuwa  makamu wa Kiongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato ulimwenguni amefariki Jumapili, Mei 21, 2023, huko Colorado Springs, Colorado, Marekani.

Akiwa na umri wa miaka 74 Schoun alikuwa kiongozi  Kanisa la Waadventista wenye uzoefu. Kiongozi ambaye alijulikana kwa mtazamo wake sawia na umakini mkubwa katika usimamizi na utatuzi wa migogoro.

Schoun alimaliza Shahada ya Uzamili ya Elimu ya  Uungu mwaka 1972 na Shahada ya Uzamivu katika Huduma za Kichungaji mwaka 1981 katika Seminari ya Kitheolojia ya Chuo Kikuu cha Andrews huko Berrien Springs, Michigan, Marekani.

Tasnifu yake katika taaluma hiyo ikawa ni upatikanaji wa kitabu cha nyenzo ya kuunda mfumo wa msaada kwa wachungaji wa kanisa hilo.

Kuanzia 1972 hadi kustaafu kwake katika mwaka 2015, Schoun alihudumu katika nyadhifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mchungaji wa kanisa nchini Marekani na Kanada, profesa wa chuo, na msimamizi wa elimu na uongozi wa kanisa.

Alihudumu kwa miaka 13 katika Chuo Kikuu cha Andrews akiwa ni  profesa wa uongozi wa kanisa, mkurugenzi wa Kituo cha Elimu Endelevu na  Huduma, na mkuu msaidizi wa Seminari ya Theolojia.Umaalumu wake ulikuwa katika usimamizi wa uongozi wa kanisa na usimamizi wa migogoro.

Mnamo 1998, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti  wa Konferensi ya New England  Kaskazini ya Kanisa la  Waadventista wa Sabato, na miaka miwili baadaye, akawa Mwenyekiti wa Unioni ya  Atlantiki zote za nchini Marekani.

Redio ya Waadventista Ulimwenguni (AWR) ilimchagua kuwa rais wake mwaka wa 2002, nafasi ambayo alishikilia hadi 2010,ambapo pia alikuwa akihudumu katika makao makuu ya Kanisa hilo.

Wakati wa uongozi wake akiwa Rais wa AWR, idadi ya lugha za matangazo iliongezeka kutoka 45 hadi zaidi ya 75, na AWR ilianza kutumia vituo vingi vya FM duniani kote ikiwemo Morning Star Radio ya jijini Dar es salaam,Tanzania  pamoja na kuendelea na matangazo yao ya awali ya mawimbi ya masafa mafupi.SW

Mnamo 2010, Schoun alichaguliwa kuwa makamu wa Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni  nafasi ambayo alishikilia hadi kustaafu kwake miaka mitano baadaye.

Katika nafasi hii, alifanya kazi kwa karibu na vyombo vya habari vya Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni, ikiwa ni pamoja na AWR, Hope Channel, Adventist Review, na Idara ya Mawasiliano ya Makao Mkuu ya Kanisa hilo.

Mara kadhaa alizuru Barani Afrika na mara ya mwisho kutembelea Tanzania ilikuwa mwaka 2014 ambapo alikuwa miongoni mwa Viongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni walioshiriki tukio la kuchangia Hope Channel Tanzania wakati huo ikiitwa Morning Star TV lililofanyika katika viwanja vya maonesho ya Sabasaba PTA jijini Dar es salaam Aprili 19.

Pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Andrews na Mwenyekiti wa Bodi ya Kimataifa ya Huduma za Kichungaji na Elimu ya Theolojia.

Schoun ameacha mke wake Carol na binti mkubwa aitwaye Kelly. Mazishi yake yalifanyika kifamilia pekee.No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.