WATU WENYE SILAHA WAVAMIA KANISA LA WAADVENTISTA WA SABATO
Ibada ya Sabato ya Novemba 26 ,2022 ilikatizwa katika Kanisa la Waadventista wa Sabato Johannesburg Central nchini Afrika Kusini mwishoni mwa juma na genge la wanaume sita wenye silaha ambao waliwashikilia mateka waumini, wakiwaibia washiriki pesa taslimu na vitu vingine vya thamani.
Video fupi isiyozidi sekunde 30 iliyonaswa mwanzo wa tukio hilo kanisani hapo inamuonesha mhubiri akitambua kinachoendelea, anasimamisha mahubiri, na kuketi chini huku ikionekana kuwa kuwa anaelekezwa cha kufanya na mmoja wa washiriki wa genge hilo la wahalifu.
Kwa mujibu wa News24, msemaji wa polisi Kanali Noxolo Kweza alieleza kuwa kuwa “Waliwatishia waumini wa kanisa hilo kwa bunduki. Hakuna aliyejeruhiwa na hakuna aliyekamatwa bado. Baadaye washukiwa walitoka nje ya kanisa hilo.” Polisi bado wanawasaka washukiwa hao wenye silaha.
Kaimu Kamishina Mkuu wa Jimbo la Gauteng Meja Jenerali Tommy Mthombeni alilaani shambulio hilo dhidi ya kanisa akisema, “Polisi watafanya kila linalowezekana kuwatia hatiani wahusika. Washiriki wa kanisa wanapaswa kuruhusiwa kufanya shughuli zao kwa amani.”
Ukurasa wa Facebook wa Kanisa la Waadventista wa Sabato la Johannesburg Central ulikuwa na chapisho baada ya tukio lililosomeka''Nashukuru Mungu hakuna aliyeumia ila watu waliachwa na kiwewe. Warumi 12:19-21 -Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu; mimi nitalipa, asema BWANA.'' Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mnyweshe; maana kwa kufanya hivyo utampalia makaa ya moto juu ya kichwa chake.
Chapisho la baadaye la Facebook katika ukurasa huo lilitoa huduma za ushauri nasaha kwa waumini, pamoja na maombi na usaidizi,kuhimiza washiriki kusaidiana na kuwahakikishia kwamba "hili pia litapita."
Post a Comment