WAADVENTISTA WATAKA HESHIMA NA UTU KWA WAHAMIAJI MAREKANI
Uongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato katika Divisheni ya Amerika ya Kaskazini (NAD) umetoa tamko la kusikitishwa kuhusu matukio ya vurugu wakati wa ukamataji wa wahamiaji yanayotekelezwa na shirika la serikali ya Marekani linalohusika na utekelezaji wa sheria za uhamiaji na usalama wa mipaka (ICE) humo, Marekani ni moja ya nchi zilizoko katika Divisheni hiyo.
Ujumbe wa tamko hilo la uongozi umetolewa kupitia kurasa rasmi za mitandao ya kijamii na tovuti ya NAD ukieleza kusikitishwa kwake na kuongezeka kwa matukio ya vurugu miongoni mwa jamii za wahamiaji walioko katika makanisa na shule za kanisa huko Minnesota na maeneo mengine nchini Marekani.
" Kadiri matukio ya vurugu yanavyozidi kuongezeka, wahamiaji wengi katika jamii zetu na ndani ya makanisa na shule zetu wameathiriwa kwa kiwango kikubwa. Tunasikitishwa na hali hii na pia tunasononeshwa sana na matukio ya hivi karibuni ya matumizi ya nguvu hatari na majeraha mabaya yanayoathiri familia na jamii huko Minnesota na maeneo mengine ya Marekani, ambayo yameongeza hofu na huzuni.Tukiongozwa na imani katika utakatifu wa uhai wa mwanadamu, Divisheni ya Amerika Kaskazini inatoa tena wito huu ili kuthibitisha upya dhamira yetu ya kiimani ya kuheshimu utu wa binadamu, heshima, na huruma kwa wote. Tunaomba amani na hekima katika nyakati hizi zenye misukosuko" umeeleza ujumbe huo.
Nchini Marekani, mabadiliko makubwa ya sera za uhamiaji yameanza kushuhudiwa kufuatia kuingia madarakani kwa Rais Donald Trump. Serikali mpya imeweka mkazo katika kuongeza ukaguzi na utekelezaji wa sheria za uhamiaji, hatua inayojumuisha kuimarishwa kwa operesheni za ICE katika ukamataji wa watu wasio na vibali katika maeneo mbalimbali.
Januari 2025 Divisheni ya Amerika Kaskazini (NAD) ilitoa mwongozo kwa wachungaji na viongozi wa makanisa na shule nchini Marekani,wenye kurasa nne kuhusu sera mpya za uhamiaji zilizopitishwa na serikali iliyoko madarakani kuhusu kuondoa unyeti wa makanisa na shule za kanisa nchini Marekani na hivyo makanisa ya waadventista hayatakuwa na uangalizi maalumu kama ilivyokuwa kabla.
NAD inajumuisha nchi tatu, Takwimu zikionesha kuwa Marekani ndiyo yenye zaidi ya asilimia 90 ya waumini wa kiadventista, kati yao asilimia 30 hadi 40 ni wahamiaji ama watoto wa wahamiaji.
Kumekuwa na mijadala kufuatia taarifa za matukio ya vurugu na vifo vinavyohusishwa na operesheni za kukamata wahamiaji wasio na vibali. Ripoti zinaonyesha kuwa baadhi ya wahamiaji wamejeruhiwa wakati wa kukamatwa, katika vituo vya kizuizini, au wakati wa operesheni za ufuatiliaji. Matukio haya mara nyingi huibuka wakati wa makabiliano kati ya maafisa wa ICE na watu wanaojaribu kukimbia au kupinga kukamatwa, huku uchunguzi wa ndani ukianzishwa ili kubaini chanzo na hatua zinazofaa kuchukuliwa.

.png)
Post a Comment