MTANGAZAJI

TAASISI ZA UMMA ZAAGIZWA KUTUMIA MFUMO WA TANePS

 


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande, ameziagiza taasisi zote za umma zilizosajiliwa katika Mfumo wa kielektroniki wa  Ununuzi wa Umma (TANePS) kuutumia mfumo huo kwa kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali ili kutoiingiza Taifa katika hasara.

Maagizo hayo yametolewa jijini Dodoma wakati wa akipokea Ripoti ya Tathmini ya Utendaji katika Ununuzi wa Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Alisema kuwa  wote wanaokwepa kutumia mfumo wa TANePS  ni wabadhilifu kwa kuwa Serikali imetumia gharama kubwa kuanzisha mfumo huo kwa lengo la kudhibiti mianya ya rushwa katika ununuzi.   
“Kuna baadhi ya taasisi za umma hazitaki kutumia mfumo, Serikali haitovumilia taasisi hizo au mtu yoyote atakae onesha kiashiria cha ubadhilifu wa mali za umma”, alisisitiza Chande.
Alisema uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango utakutana na uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ili kuona namna bora ya kushughulikika na taasisi zilizoshindwa kukidhi matakwa ya sheria.
Chande alisema pia kumekuwepo na ubadhilifu wa fedha za umma wakati wa ununzi kutokana na baadhi ya watumishi kutokuwa na weledi na uaminifu na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchua hatua kali kadiri itakavyokuwa inawabaini.
Aidha, aliipongeza PPRA kwa kuweza kusimamia Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura Na. 410 kwa kuandaa na kuwasilisha ripoti ya kina ya utendaji kazi wa Sekta ya ununuzi wa umma nchini.
Awali akiwasilisha Ripoti ya Tathmini ya Utendaji katika Ununuzi wa Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/22, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PPRA, Dkt. Leonada Mwagike, alisema kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2021/22, kati ya zabuni 62,161 zilizopangwa kufanyika, zabuni 47,424 ndizo zilichakatwa ndani ya mfumo ikiwa ni asilimia 76.29, jambo linaloonesha baadhi ya zabuni hazikufanyika ndani ya mfumo.
Alisema kuwa katika mwaka wa fedha huo jumla ya taasisi 803 ziliunganishwa katika mfumo wa TANePS na jumla ya wazabuni 8,447 walisajiliwa ili kuutumia mfumo huo na hivyo kufanya jumla ya wazabuni waliosajiliwa kufikia 30,020.
Aidha jumla ya taasisi nunuzi 667 kati ya taasisi 803 zilipandisha mipango yao ya mwaka ya ununuzi (Annual Procurement Plans) ndani ya mfumo wa TANePS ambapo mipango hiyo ilikuwa na zabuni 62,161 zenye gharama ya shilingi trilioni 32.1.
Vilevile alieleza kuwa ripoti iliyowasilishwa inajumuisha matokeo ya ukaguzi uliyofanywa na PPRA katika taasisi mbalimbali ili kupima kiwango cha uzingatiaji Sheria na pia upatikanaji wa thamani halisi ya fedha ambapo jumla ya taasisi nunuzi 232 zilifanyiwa ukaguzi.
Dkt. Mwagike alisema, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyoimefanya ukaguzi huo kupitia mfumo wa TANePS. Ukaguzi huo ulihusisha kundi la Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala (MDAs) 128, Mamlaka za Serikali za mitaa (LGAs) 26 na mashirika ya umma 78 ambapo jumla ya zabuni 2,156 zenye thamani ya shilingi trilioni 8.62 zilikaguliwa.
Alibainisha kuwa matokeo ya ukaguzi yalionesha kiwango cha ukidhi wa Sheria kilikuwa cha wastani wa asilimia 65 ambacho ni kiwango cha chini ukilinganisha na matarajio ya asilimia 80.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.