MTANGAZAJI

SAMIA SCHOLARSHIP HII HAPA

 


Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefungua dirisha la maombi ya SAMIA  SCHOLARSHIP kwa wanafunzi 640 waliopata ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi katika mitihani ya Kidato cha Sita 2022.
Majina ya wanafunzi hao yanapatikana kuanzia leo katika tovuti ya wizara www.moe.go.tz na ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu www.heslb.go.tz.  Aidha wanafunzi hao wataanza kuomba ufadhili huo kuanzia  Septemba 28, 2022  kupitia tovuti ya Bodi ya Mikopo ya Mikopo https://olas.heslb.go.tz kwa siku 14.
Akitoa tangazo hilo Septemba 27, 2022 jijini Dodoma Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema wanafunzi hao watafadhiliwa kwa asilimia mia moja kwa kipindi cha miaka mitatu hadi mitano kulingana na programu husika walizodahiliwa.
Amefafanunua kwamba wanafunzi hao ni wa Tahasusi za sayansi ambazo PCB, PCM, PGM, CBG, CBA, PMC na CBN.
 "SAMIA SCHOLARSHIP itagharamia kwa asilimia mia moja masomo ya Chuo Kikuu kwa wanafunzi ambao wamepata udahili katika fani za Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba katika Vyuo vikuu vya Tanzania  vinavyotambulika na Serikali ," amesema Prof. Mkenda
Ufadhili huo utazingatia viwango na miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa kugharamia ada ya mafunzo, posho ya chakula na malazi, vitabu na viandikwa, mahitaji maalum ya vitivo, mafunzo kwa vitendo, utafiti, vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na bima ya Afya.
Prof. Mkenda ametaja masharti saba ya ufadhili huo ikiwemo kiwango cha ufaulu wa mnufaika kisiwe chini ya GPA 3.8 katika mwaka wa masomo na chini ya hapo ufadhili utasitishwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Ali Abdulgullam Hussein amepongeza hatua ya Serikali kutoa ufadhili huo  ambapo kwa upande wa Zanzibar ufadhili wa aina hiyo pia umetolewa kwa wanafunzi 30 hivyo kuongeza fursa kwa watoto wa Kitanzania kupata elimu ya juu.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.