MTANGAZAJI

WATUMIA MITANDAO YA KIJAMII TANZANIA NI WAHANGA WA UKATILI MITANDAONI

 


Katibu Mkuu Wizara ya  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula, amesema asilimia nne kati ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaokadiriwa kufikia Milioni  54 nchini Tanzania  kwa sasa wanakabiliwa na ukatili mitandaoni.

Akizungumza jijini Dodoma hivi karibuni kwenye kikao kazi kilicho washirikisha kikosikazi cha Taifa, kutoka Asasi za kiraia pamoja na Serikali, Dkt. Chaula amesema pamoja na ukuaji wa teknolojia bado kunatakiwa kuongeza mbinu na mikakati katika kuchukua hatua za kukabiliana na ukatili mitandaoni kwakuwa matumizi ya teknolojia yamekuwa na athari za ukatili, kwa watumiaji wasiokuwa na uwelewa.

“Sisi humu ndani unaweza kukuta wote ni wahanga wa ukatili wa mitandaoni, leo tunaandaa vitini kwaajili ya watoto lakini tukumbuke ukatili huo sio kwa watoto tu bali hata watu wazima” amesema Dkt. Chaula.

Dkt. Chaula amekielekeza kikosi kazi hicho kuwajumuisha viongozi wa dini, wanahabari na makundi mengine yenye ushawishi ndani ya jamii katika kupiga vita ukatili mitandaoni kwakuwa, watu viongozi wa dini wao kwa nafasi zao kwenye mahubiri yao inakuwa ni sehemu ya mafundisho, lakini wanahabari ninyi ni kundi muhimu sana katika kutengeneza vipindi vya kutoa elimu

Akichangia kwenye kikao hicho, Mbunge wa Viti Maalum, na mdau wa kupambana na Ukatili, Neema Lugangira, amesema pamoja na kuwa na idadi  ya wabunge wanawake zaidi ya 140 lakini idadi ya wanaotumia wa mitandao ni ndogo,  hata kama wanafika kumi na tano lakini ukiwauliza kulikoni wanasema wanahofia ukatili wa mitandaoni.

Awali akielezea malengo ya kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Sebastiani Kitiku amesema wametumia siku mbili kwenye kikaokazi hicho ambapo nyaraka hizo watakazo toka nazo zitawasaidia watoto kujilinda na ukatili wa mitandaoni.

“Ndugu wajumbe tumesikia maelekezo ya Katibu Mkuu, kuwa miongozo hii tuwafikishie wadau wakiwepo viongozi wa dini lakini kama kikosi kazi tumeenda mbali zaidi kwamba miongozo hii tutaifikisha hadi mashuleni kwa walimu kwani tunaimani wao hukaa na watoto muda mwingi hivyo tutatumia jukwaa hilo na majukwaa mengine ili elimu hii isambae zaidi”. alisema Kitiku.

Nao wajumbe wa Baraza la watoto ambao nisehemu ya kikosikazi hicho wamesema, wao kama  watoto, kwanza wanaona fahari kwa Serikali yao kuwajali kwa kuwaandalia mwongozo, lakini wanataka Mwongozo huo, lazima kwanza ueleweke pia kwa wazazi.

“Utakuta mzazi amechukua simu yake pengine mpo kweye Sherehe anakupiga picha na kusambaza kwa rafiki zake, ukimwambia Baba au Mama mimi sitaki anakwambia kwani mimi si ndio ninaye kujua, hivi kwakweli sio vizuri tunaomba watusikilize kwa maana na sisi tunahaki zetu za msingi. Alisema Cayleen Nelson, Mwakilishi wa Baraza la Watoto Dodoma.

Matokeo ya kikao hicho yanatokana na tafiti iliyofanywa baina ya Serikali na wadau UNICEF, kuona maeneo ya kipaumbele yakuanzia kwenye kukabiliana na ukatili mitandaoni, ambapo imebainika sio watoto peke yao ambao ni wahanga bali pia watu wazima, hivyo kukamilika kwa kikao hicho kitatoka na vitini ambayo vitakuwa ni miongozo kwa makundi hayo.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.