SHERIA ZINAZOWAHUSU WAMACHINGA KUTAFSIRIWA KWA KISWAHILI
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Shirikisho la Umoja wa
Wamachinga (SHIUMA), imeazimia kuhakikisha sheria ndogo zinazowahusu
wamachinga zinatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili Wamachinga wote
waweze kuzielewa.
Maazimio
hayo yamefikiwa wakati wa kuhitimisha kikao cha siku mbili kati ya
Wizara na Viongozi wa SHIUMA kutoka Mikoa ya Tanzania Bara
kilichoongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula kilichofanyika Jijini
Dodoma.
Akifunga kikao
hicho, Dkt. Chaula amewataka Wamachinga kushirikiana na Serikali
kutekeleza maazimio waliyojiwekea kwa wakati kwa maslahi yao na Taifa
kwa ujumla.
" Kufikia Machi 16 wanasheria wa SHIUMA kwa kushirikiana na wanasheria wa
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na
Ofisi ya Rais TAMISEMI wakamilishe kutafsiri Sheria hizo" amesema Dkt.
Chaula.
Dkt. Chaula
ameyataja maazimo ya kikao hicho kuwa ni pamoja na Wizara ya Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum iboreshe madawati ya
kushughulikia masuala ya Wamachinga kwa kushirikiana na Ofisi Rais
TAMISEMI hadi Halmashauri, ili kusaidia kutatua changamoto kwenye maeneo
yao.
Ameyataja maazimio
mengine kuwa ni Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI
kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zinapanga na kuweka miundombinu
wezeshi katika maeneo ya shughuli za Wamachinga kwa kushirikiana na
Viongozi wa Wamachinga wa eneo husika, kuandaa kanzidata ya Wamachinga
na Wizara kutembelea maeneo ya masoko ya Wamachinga ili kutatua
changamoto zilizopo.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa SHIUMA Taifa, Ernest Matondo ameishukuru
Serikali kwa kuwakutanisha Wamachinga na kuahidi kushirikiana na
Viongozi pamoja na Wamachinga mikoa yote ili kufanikisha kufika mbali na
kutoka katika umachinga na kuwa wafanyabishara wa kati na wakubwa.
Naye
Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI
Nuru Namoroma amewahakikishia Wamachinga wote kuwa Ofisi hiyo itaendelea
kuratibu masuala yao kwa ufanisi zaidi katika ngazi ya Serikali za
Mitaa kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake
na Makundi Maalum ili wawe na mazingira mazuri ya kufanya biashara.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa
kushirikiana na SHIUMA kuratibu maadhimisho ya wiki ya Wamachinga
itakayofanyika tarehe 29 Juni kila mwaka.
Post a Comment