BILIONI 48.4 ZA TOZO MIAMALA YA SIMU ZAKUSANYWA NDANI YA WIKI NNE
Serikali ya Tanzania imewaomba watanzania kuwa na subira wakati ikiendelea kushughulikia suala la tozo ya miamala ya simu na kutoa taarifa ya makusanyo ya fedha za tozo hizo katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita ambapo makusanyo yalikuwa zaidi ya shilingi bilioni 48.4 ambazo zimepelekwa kwenye miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Akitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Mipango, Mwingulu Lameck Nchemba alisema kati ya kiasi hicho cha fedha, shilingi bilioni 22.5 zimepelekwa TAMISEMI kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 90, na kuahidi kupeleka kiasi kingine cha sh. bilioni 15 mwezi Agosti, 2021 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vingine 60 na kufanya idadi ya vituo vitakavyojengwa kufikia 150 nchi nzima.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango- Zanzibar Dkt. Juma Malik Akil, alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar, katika kipindi cha wiki nne tangu kuanza kutozwa kwa tozo za miamala ya simu, Serikali imekusanya shilingi bilioni 1.6 ambazo zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo Visiwani humo.
Alhamisi Julai 15, 2021, watumaji na watoaji fedha kupitia simu za mkononi nchini Tanzania walianza kulipa kodi ya uzalendo iliyopandisha gharama za kutuma na kutoa fedha mara 11 ya ilivyokuwa mwanzo, hali iliyoelezwa kuacha maumivu kwa wengi.
Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema tozo mpya ni mzigo mwingine kwa wenye kipato cha chini, hasa vijijini ambako simu za mkononi ni mkombozi wa huduma za fedha kutokana na kutokuwepo kwa huduma za benki.
Naye Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile, aliwahakikishia watanzania kuwa kikosi kazi kilichopewa majukumu ya kupitia upya gharama za tozo hizo kinaendelea kuchakata maagizo hayo na ndani ya mda mfupi watatoa mapitio yatakayotoa mwelekeo mpya katika hizo tozo na kuwaomba wa Tanzania kuendelea kuwa na subira na jambo hilo.
Post a Comment