MTANGAZAJI

MAABARA YA TEKNOHAMA NKOLOLO NI KITENDAWILI

 

 
Mbunge wa Bariadi na  Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania Mhandisi Kundo Mathewa amesikitishwa na uongozi wa Kata ya Nkololo kwa kushindwa kusimamia ujenzi wa maabara ya TEKNOHAMA katika shule ya Sekondari Nkololo wilayani Bariadi wakati tayari Mbunge huyo alikwishapeleka mifuko 156 ya saruji na mabati 50 toka mwezi Machi, 2020 lakini mpaka sasa hakuna chochote kilichofanyika zaidi ya kufyatua tofali 1500.
 
Waziri huyo alitoa kauli ya hiyo wakati wa kukabidhi vifaa vya TEKNOHAMA vilivyotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini Tanzania (UCSAF) kwa Shule ya Sekondari Dutwa na Shule ya Sekondari Nkololo zilizopo katika Wilaya ya Bariadi ambavyo ni kompyuta 10 na printa 2 ambapo kila shule imepatiwa kompyuta 5 na printa 1.

“TEKNOHAMA inaenda kuchangia kukuza uchumi wa dunia na sisi Tanzania tumeona kwamba tusibaki nyuma katika kukuza matumizi ya TEKNOHAMA kwa kuhakikisha vijana wetu wanajifunza TEKNOHAMA kuanzia shuleni na nikiwa kama Mbunge wa Bariadi nina kila sababu ya kuwasisitiza vijana wetu
kusoma kwa bidii”, amezungumza Mhandisi Kundo.
 
 Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri na Wataalam wake wahakikishe wanatoka ofisini na kwenda kuweka kambi katika shule hiyo ili kusimamia ujenzi wa darasa hilo hadi ukamilike.

“Baada ya hapa nataka nipate maelezo kwanini darasa halijakamilika kutoka mwezi Machi mpaka sasa na wakati vifaa vyote vipo, nani alikuwa anasimamia, nani alipinga na nani alichelewesha na taarifa hiyo niipate ndani ya wiki moja” alizungumza Kapange.
 
 Iliamuliwa kuwa vifaa vya TEKNOHAMA vilivyopelekwa kwa ajili ya Shule ya Sekondari Nkololo vihifadhiwe na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mpaka hapo chumba cha maabara ya TEKNOHAMA ya shule hiyo kitakapokamilika ndio
 
Kwa Upande wa Mkuu wa Uendeshaji wa UCSAF Mhandisi Albert Richard amesema moja ya majukumu yanayotekelezwa na Mfuko huo ni kupeleka vifaa vya TEKNOHAMA katika shule za umma ili kuendelea kuinua matumizi ya TEKNOHAMA nchini Tanzania.
 
Mwalimu Mekrina Bonifasi wa Shule ya Sekondari Dutwa amesema kuwa msaada huo wa kompyuta utakuwa chachu ya ufaulu na utasaidia sana katika ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi hasa ukizingatia kuwa kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi wa kidato cha kwanza wapatao 280 ambao wanasoma somo la kompyuta na watafanya mtihani wa Taifa 2022 kwa mara ya kwanza.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.