MTANGAZAJI

WAZIRI ATAKA WASIOLIPA KODI WAONDOLEWE

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile amelitaka Shirika la Posta Tanzania kukusanya madeni kutoka kwa watu wote wanaotumia milki za Shirika (wapangaji) ikiwemo wa majengo na viwanja kulipa kodi zao ndani ya miezi mitatu na kinyume cha hapo hatua za kuondoa watu hao zichukuliwe.

 “Watu wote wanaokaa kwenye milki za Shirika wanapaswa kulipa kodi nawatu ambao hawajalipa waondolewe,nakupa miezi mitatu, kuhakikisha wenye madeni wawe wamelipa kikamilifu kwa sababu hatuwezi kuona watu wanatumia rasilimali za Shirika na hawalipi” Alisema Dkt. Ndugulile. 

 Ameyasema hayo wakati akifanya kikao kazi na Menejimenti ya Shirika la Posta Tanzania mara baada ya kufanya ziara yake ya kikazi kutembelea ofisi, milki na rasilimali zinazomilikiwa na Shirika hilo, Dar es salaam pamoja na kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa kwa Menejimenti hiyo alipolitembelea Shirika mwezi Januari, 2021.

 Amelitaka Shirika kubadilika ili kuendana na kasi ya sasa ya dunia ilikuendana na matakwa na mahitaji ya wananchi kwa kujikita zaidi kwenye mabadiliko ya utendaji, mikakati, mitazamo ndani ya taasisi pamoja na bidhaa na huduma zinazotolewa na Shirika kwa wananchi.

 Sambamba na hilo amewataka wafanyakazi wa Shirika hilo kutimiza majukumu yao kwa wakati na hasa kuhakikisha ufanisi katika maeneo wanayosimamia kwa lengo la kuleta matokeo chanya kwa taasisi na taifa kwa ujumla na amesisitiza ushirikiano katika maeneo ya kazi kwa kuwa wafanyakazi wote wanawajibika kwa umma na sio mtu binafsi hivyo italeta ufanisi.

 “Sipendi kutuma mtu kazi nataka kila mtu ajitume kwenye majukumu yake katika eneo analolisimamia ahakikishe anawajibika katika kuleta matokeo chanya ndani ya taasisi yetu jengeni ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja katika kuyatimiza haya”. Alisisitiza Dkt. Ndugulile.

 Kwa upande wake Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika hilo Macrice Mbodo amemshukuru Dkt. Ndugulile kwa kutenga muda wake na kuja kuwatembelea na ameyapokea maagizo yaliyotolewa na kwa kushirikiana na Menejimenti ya Shirika ameahidi kuyafanyia kazi usiku na mchana katika kuhakikisha malengo ya Shirika na Serikali yanafikiwa.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.