MTANGAZAJI

SERIKALI YA TANZANIA YAKARIBISHA SEKTA BINAFSI KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO

 Serikali ya Tanzania imefungua wigo kwa sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ili kufanikisha utekelezaji wa malengo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26 unaotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania  Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alipokutana na wadau na taasisi za fedha nchini humo  katika kikao kilichoangazia ugharamiaji wa miradi ya maendeleo kwa njia mbadala.

Akizungumza katika kikao hicho Dkt. Nchemba alisema kuwa tathmini iliyofanyika ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendelo wa Taifa ilibainisha ushiriki mdogo wa sekta binafsi katika utekelezaji wa mpango huo hivyo Serikali imeona ijadiliane nao kuona namna bora ya kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo.

Alisema kuwa kuna umuhimu wa kuwa na njia mbadala za kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ili isiathiri utekelezaji wa shughuli za utoaji wa huduma za kijamii, ikiwemo elimu, maji na afya.

Alifafanua kuwa kwa upande wa miradi inayoweza kutekelezwa kwa njia mbadala Serikali itaboresha mazingira ya kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo kupitia sekta binafsi kwa kuhakikisha inafanyia kazi baadhi ya hoja zilizoibuliwa katika kikao hicho ikiwemo masuala ya kiutawala.

Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Dk. Charles Mwamwaja alisema kuwa dirisha hilo litatoa fursa kwa Serikali kupata fedha kutoka vyanzo vya ndani kutatua changamoto ya upatikanaji wa fedha za miradi na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo itakayojumiisha maeneo mengi zaidi.

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa hilo  umebainisha kiwango cha fedha kitakachohitajika katika utekelezaji wa miradi ambapo Serikali inatarajia kukusanya kiasi cha Sh. trilioni 74.3 katika vyanzo vyake na kiasi cha Sh.40.6 kinatarajiwa kupatikana kutoka vyanzo mbadala ikiwemo Sekta Binafsi. 


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.