MTANGAZAJI

RAIS SAMIA NA KENYATTA KATIKA UTATUZI WA VIKWAZO.
Marais wa Tanzania na Kenya wametangaza kuwa nchi hizo mbili zimeingia makubaliano ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka jiji la Dar es Salaam mpaka Mombasa. 

Rais wa Tanzania Samia yuko nchini Kenya kwa ziara rasmi ya siku mbili ikiwa ni mwaliko wa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta tangu Rais huyo kushika madaraka baada ya aliyekuwa Rais wa Tanzania awamu ya tano Hayati John Magufuli kufariki dunia.

Katika hotuba zao kwa waandishi wa habari baada ya kufanya kikao cha faragha katika Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta pamoja na mgeni wake Rais Samia wa Tanzania wamesema kuwa bomba hilo litakuwa muhimu katika maendeleo ya nchi zote mbili.

Kwa upande wake Rais Samia ameeleza kuwa baada kuingia mkataba huo kilichofuata sasa ni kusimamia utekelezaji wa makabaliano hayo kwa pande zote mbili.

Tanzania imegundua gesi katika mikoa yake ya pwani ya kusini ya Lindi na Mtwara na tayari gesi hiyo imefikishwa katika jiji la Dar es Salaam ambapo imeunganishwa na viwanda kadhaa lakini pia inatumika kuzalisha umeme unaoingia moja kwa moja katika gridi ya taifa. 

 Marais hao wawili pia wameeleza kuwa wamejadiliana kuhusu kurahisisha ufanyaji wa biashara baina ya nchi hizo mbili.

Rais Kenyatta amesema kuwa wamekubaliana kuwa Tume ya Pamoja ya mawaziri wa nchi hizo mbili iwe inakutana mara kwa mara ili kutatua changamoto za kibiashara na uhusiano zinatazotokea huku Rais Samia akieleza kuwa wamekubaliana kuondosha vikwazo visivyo vya kikodi katika biashara ya mpakani.

Samia ameeleza kuwa  Kenya ni nchi ya tano kwa kuwekeza nchini Tanzania na ya kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki. Makampuni zaidi ya 400 ya Kenya yamewekeza dola bilioni 1.7 na kuna makampuni ya Kitanzania yamewekeza Shilingi za Kenya Bilioni 19 na kuahidi kuwa kampuni kutoka Tanzania zitaongeza nguu zaidi kuwekeza Kenya.

 Kwa upande wa mapambano dhidi ya maambukizi ya Corona, Rais Samia amesema wamekubaliana na Rais Kenyatta kuwa mawaziri wa afya wa nchi hizo wakutane kuangalia namna ya kurahisisha mfumo wa  kupima na hasa  katika mipaka ya nchi hizo mbili.

 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.