MTANGAZAJI

UANZISHWAJI WA VITUO VYA MALEZI YA WATOTO KIJAMII TANZANIA

 

Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Mwajuma Magwiza(mwenye hijab) akiwa na timu ya wataalam kutoka Wizara hiyo na TAMISEMI wakiangalia mradi wa ujenzi wa Kituo cha Malezi ya watoto wadogo kinachoshirikisha Jamii, Serikali na Shirika la Brac kilichopo katika Shule ya Msingi Rufu, Manispaa ya Temeke jijini Dar Es Salaam.

 

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Shirika la Brac Tanzania imeanza kuratibu uanzishwaji wa Vituo vya Malezi kwa watoto wadogo vitakavyomilikiwa na kuendeshwa na Jamii ya eneo husika.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Mwajuma Magwiza ametoa taarifa hiyo wakati akikagua Maendeleo ya uanzishwaji wa vituo hivyo kwa Halmashauri za Wilaya ya Temeke na Kigamboni vinavyojengwa kwa ushirikiano wa Wananchi, Serikali na Shirika la Brac.

 

Bi. Mwajuma amesema lengo la uanzishwaji wa Vituo vya Malezi kwa watoto katika kijamii ni kuhakikisha watoto wanapata sehemu sahihi ya kukaa na kulelewa wakati wazazi na walezi wanapokuwa katika majukumu ya kutafuta riziki.

 

Ameongeza kuwa vituo hivyo vya Malezi pia vitasaidia kuondokana na vitendo vya Ukatili kwa watoto wadogo ikizingatiwa kuwa watoto hao hufanyiwa vitendo vya Ukatili katika jamii zetu.

 

" Vituo hivi vitakuwa chini ya jamii husika na vitasaidia malezi kwa watoto pale wazazi na walezi wanapokuwa katika majukumu ya utafutaji wa kipato" alisema

 

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbagala Kuu Fabian Chilumba amesema kuwa wameupokea mradi huo kwa dhati na atahakikisha anahamasisha wananchi waendelee kuchangia nguvu zao kuhakikisha mradi inaisha kwa wakati na kuanza kutumika.

 

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Somangila na Naibu Meya Manispaa ya Kigamboni Mhe. Steven Warioba amesema kuwa kuna uhitaji mkubwa wa vituo hivyo katika Mitaa kwani kuna watoto wengi wanahitaji huduma ya uangalizi wakati wazazi hawapo nyumbani.

 

 

Serikali ya Tanzania  kwa kushirikiana na Shirika la Brac na wananchi kuchangia nguvu zao inaendesha zoezi la ujenzi wa mradi wa Vituo vya Malezi kwa Watoto wadogo kwenye ngazi ya Jamii katika mikoa ya Dodoma na Dar Es Salaam ambapo, jumla ya Vituo 30 vinajengwa katika Mitaa ya Halmashauri mbalimbali za mikoa hiyo.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.