TIKETI ZA USAFIRI WA TREN SASA KUPITIA AIRTEL MONEY
Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania imetangaza ushirikiano mpya na Shirika la Reli Tanzania kupitia huduma yake ya Airtel Money ambapo kuanzia sasa, wateja wao wataweza kununua tiketi za kusafiri wa treni kupitia akaunti zao za Airtel Money.
Kwa sasa, usafiri wa treni umekuwa ni mkombozi kwa watanzania baada ya serikali kuimarisha sekta ya miundombinu ya reli nchini kwa kukarabati reli ya kanda kaskazini (Tanga, Moshi, Arusha) na huduma hii inaanzia Dar es salaam -Arusha.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kutangaza ushirikiano huo mpya, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Airtel Tanzania Mkurugenzi wa mawasiliano wa Airtel Bi, Beatrice Singano alisema kuwa Airtel Money imekuwa tayari kukaribisha ushirikiano wowote ambao unaongeza tija kwa wateja wake.
" Wateja wa TRC kwa sasa wataweza kulipia tiketi zao kupitia huduma yetu ya Airtel Money kwa uhuru kabisa. Naomba nitumie fursa hii kutoa rai kwa wateja wa Airtel kutumia huduma yetu ya Airtel Money ili kuokoa muda na kufanya malipo kwa njia rahisi na salama".
Amesema wanaelewa kuwa hiki kipindi cha msimu wa sikukuu wateja wao husafiri sana kwa ajili ya kwenda kukutana na familia, ndugu jamaa na marafiki kwa ajili ya kusherehekea sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya.
Singano amesema ushirikiano huu utawapa unafuu kwani kwa sasa watakuwa na uhuru wa kulipia tiketi za usafiri wakiwa mahali popote pale bila kutembelea ofisi za TRC,Mteja atakakiwa kupiga *150*60# kisha kwenda namba 5 Lipabili namba 5 tena Malipo ya Serikali kisha mteja ataingiza namba ya kumbukumbu aliyopata toka kwenye tovuti ya TRC na kufanya malipo papo hapo atahakikishiwa safari yake.
“Airtel Money kwa sasa imeunganishwa mtandao wa huduma kwa wateja wa Shirika la Reli Tanzania,kwa kuingia kwa tovuti ya TRC ambayo ni www.trc.co.tz, ili kukata tiketi kwa njia ya mtandao, ambapo kwa muunganiko huo wateja wa Airtel Money wanaweza kulipia tiketi zao za TRC moja kwa moja kupitia akaunti za Airtel Money kwani ni njia salama, haraka na nafuu.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa alisema TRC daima inaendeleza ubunifu katika kutoa huduma bora,haraka na salama kwa wateja wao wote kwa kuwa wanatambua umuhimu wa huduma zao kwa jamii na ni usafiri wa gharama nafuu kuliko usafiri wowote .
Kwa ubia huu na Airtel Tanzania utasaidia kuboresha zaidi utoaji huduma kwa wateja wanaotumia mtandao wakati wakulipia tiketi zao kwani ni rahisi kwenye kutumia na vile vile unaweza kujihudumia ukiwa popote na hivyo kuwahakikishia wateja huduma za uhakika na haraka za usafirishaji.
“Airtel Money ni moja ya njia rahisi na salama kwenye kufanya malipo kwa njia ya mtandao. Kwa kuwa sasa imeunganisha kwenye mtandao wetu wa malipo, wateja wetu watakuwa na uhuru wa kuchagua zaidi inapokuja suala la kulipia tiketi za usafirishaji”. Aliongezea ili kupata huduma hii wateja wanatakiwa kuingia kwa tovuti ya TRC, ambayo niwww.trc.co.tz, fungua kata tiketi kwa njia ya mtandao, unapoingia hapo utajaza kutokana ma maelekezo unapewa.
Ameendela kuwasihi wateja kukata tiketi kwa njia ya mtandao ambayo ni rahisi zaidi popote walipo, maana ni njia inayopunguza gharama na muda, huduma za usafiri wa reli kwa njia kaskazini kutoka Daresalaam -Arusha ni siku ya Jumatatu, Jumatano na ijumaa, muda wa safari kuanzia sa 8:30 mchana na inafika Arusha saa 3:00 Asubuhi, na kutoka Arusha ni Siku ya Jumanne, Alhamisi na Jumamòsi, muda ni saa8:30 mchana na kufika Dar es salaam saa 3:00 Asubuhi.
Post a Comment