MTANGAZAJI

UMOJA WA ULAYA WAISAIDIA TANZANIA BILIONI 84 KWA AJILI YA UMEME

 

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier wakisaini mkataba wa msaada wa Euro milioni 26 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 72 ikiwa ni sehemu ya msaada wa Euro milioni 30 sawa na shilingi bilioni 84 uliotolewa na Umoja wa Ulaya kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), kwa ajili ya mradi wa kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia, hafla hiyo imefanyika Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.Doto James na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) Bi. Stephanie Mouen Essombe  wakibadilishana hati za mkataba wa msaada kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) wenye thamani ya Euro milioni 26 kati ya Euro milioni 30 (sh. bil. 84) zilizotolewa na Umoja wa Ulaya kwa ajili ya mradi wa kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia.


Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), umeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 30 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 84 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kujenga miundombinu ya kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia.

 

Sehemu ya fedha hizo, kiasi cha Euro milioni 26 sawa na shilingi bilioni 72, Mkataba wake umeingiwa Jijini Dar es Salaam 15 Desemba, 2020 kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavier na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD)  Stephanie Mouen Essombe.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, amesema kuwa fedha hizo kiasi cha Euro milioni 26 kitatumika kujenga kituo cha kupooza umeme - Tunduma, kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kv 330 yenye urefu wa kilometa 4 kutoka Tunduma hadi mpakani mwa Tanzania na Zambia.

 

“Mradi huu pia unahusisha ujenzi wa njia mpya ya kusafirisha umeme katika maeneo ya vijijini, ambayo hayajafikiwa na Grid ya Taifa na kuongeza uwezo wa njia zilizopo za kusafirisha umeme kupitia Iringa – Kisada – Mbeya – Tunduma – Ushoroba wa Sumbawanga” alisema Bw. James

 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa Bi Stephanie Mouen Essombe amesema kuwa miezi michache iliyopita Shirika lake lilisaini mkataba wa mkopo nafuu wenye thamani ya Euro milioni 100 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa kusafirisha umeme wa Tanzania na Zambia.

 

“Leo tumekutana tena kwa ajili ya kusaini mkataba wa kiasi kingine cha nyongeza cha Euro milioni 26 sawa na shilingi bilioni 72 ambazo ni msaada uliotolewa na Umoja wa Ulaya kupitia Shirika letu” alisema Bi. Stephanie

 

Mradi wa kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia ni sehemu ya mwisho ya utekelezaji wa mradi wa ushoroba (corridor) kutoka Ethiopia, Kenya, Tanzania na Zambia unaolenga kupunguza gharama za matumizi ya nishati hiyo pamoja na kukuza uchumi wa nchi husika.

 

Amesema kuwa hivi karibuni, Shirika lake litatoa kiasi kingine cha Euro milioni 130 kwa ajili ya kutekeleza mradi mwingine mkubwa wa nishati jua (solar PV Power) wenye uwezo wa kuzalisha megawati 50, utakaojengwa mkoani Shinyanga.

 

Alifafanua kuwa nchi yake kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) itaendelea kuwekeza katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ambapo katika kipindi cha miaka 10 Bodi ya wakurugenzi ya AFD imeidhinisha matumizi ya kiasi cha Euro milioni 430 kwa ajili ya sekta ya nishati.

 

Naye Kaimu Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Emilio Rossetti, amesema kuwa mbali na msaada wa kiasi hicho cha Euro milioni 26 zilizosainiwa, Umoja wake utatoa kiasi kingine cha msaada wa Euro milioni 4 kwa ajili ya kulijengea uwezo Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) na kufanya kiasi kilichotolewa na EU kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kufikia Euro milioni 30 sawa na shilingi bilioni 84.

 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.