MTANGAZAJI

WABEBA MIZIGO NA WAONGOZA WATALII KILIMANJARO WALALAMIKIA MALIPO KIDOGO WANAYOPEWA NA MAKAMPUNI YA UTALII

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania Constantine Kanyasu akizungumza na wabeba mizigo na waongoza watalii kuhusu maslahi yao kiduchu wanayolipwa na baadhi ya Makampuni ya Watalii ambayo ni kinyume cha sheria wakati alipotembelea  katika Hifadhi ya Taifa ya  Mlima Kilimanjaro katika geti la Mweka kwa ajili ya kusikiliza kero zinazowakabili na kuzifanyia kazi katika ziara yake ya kikazi ya  siku mbili katika wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe. Constantine Kanyasu akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watalii wakati alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro katika geti la kuingilia la Mweka

Baadhi ya wabeba mizigo ya Watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro wamelalamika kuhusu malipo kidogo wanayolipwa na miongoni mwa makampuni ya utalii kutokana na kazi hiyo.
 
Akizungumza kwa niaba wa wabeba mizigo mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania Constantine Kanyasu mmoja wa wabeba mizigo ya Watalii   Daniel Maro ameeleza kuwa wamekuwa  wakilipwa na baadhi ya Makampuni ya watalii malipo kiduchu ya kiasi cha shilingi 5,000 na muda mwingine shilingi 8,000 badala  ya elfu 20,000 kwa siku.

Naibu Waziri huyo amefanya  ziara  ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro lengo likiwa ni kutafutia ufumbuzi kero mbalimbali zinazowakabili wadau hao katika sekta ya Utalii.
 
Maro amedai kuwa malipo hayo ni madogo sana ukilinganisha na ugumu wa kazi hiyo na wamekuwa hawana pa kulalamikia na  wale wote ambao wamekuwa wakibainika kulalamika  wamekuwa wakikosa  kupata kazi tena kutoka kwenye kampuni hayo.

Naye, Walter Mbambwo ambaye ni Muongoza watalii katika Mlima huo  amesema kutokana na tatizo la ajira wamekuwa wakilazimika kutoa rushwa ya kiasi shilingi 20,000 ili wapate kazi  hiyo lakini wamekuwa wakilipwa kiasi cha shilingi 5,000 au 8,000 tu.
 
Kwa mujibu wa sheria waongoza watalii katika mlima huo wanapaswa kulipwa si chini ya Dola 20 za Marekani kwa siku sawa na mbeba mizigo Dola 10 za Marekani kwa siku.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewashauri wabeba mizigo na waongoza watalii katika  Mlima Kilimanjaro wapunguze utitiri wa vyama walivyoviunda  vya kutetea  maslahi yao  badala yake  wabaki na vyama viwili ambavyo vitakuwa na nguvu ya kudai haki na kupigania maslahi yao.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.