MTANGAZAJI

HUYU NDIYE MGINI KWEBA MTUNZI WA NYIMBO ZA MIKUTANO YA HATIMAYE


Mgini Kweba
Mgini Kweba (wa tatu toka kulia) akiimba na waimbaji wenzake katika kundi la Vocal Praise ambalo kwa sasa halipo
Waimbaji wa Mtende walipotembelea nyumbani kwa Mgini Kweba, mbele walioketi ni Suzy mke wa Mgini na Mtoto wao wa kwanza Frank

Mkutano wa Nyumbani Hatimaye 2019 ambao ulikuwa ukifanyika Kinyerezi jijini Dar es salaam na kurushwa na Hope Channel Tanzania na Morning Star Radio na kwa udhamini wa ATAPE na TAUS unamalizika Februari 23 ,2019 ukionekana na kusikika katika sehemu mbalimbali duniani kupitia televisheni,radio,mitandao ya kijamii na program tumishi mbalimbali.

Chama cha Wajasiriamali na Wanataaluma Waadventista nchini Tanzania (ATAPE) kwa ushirikiano na Taasis ya Vyombo vya Habari vya Kanisa la Waadventista nchini humo (TAMC) wamekuwa wakirusha mikutano ya hatimaye kila mwaka ikiwa ni zaidi ya miaka mitatu sasa mbayo ni Uhuru Hatimaye,Ushindi Hatimaye,Maisha Hatimaye na Nyumbani Hatimaye.Mikutano hii hufanyika mara moja kila mwaka.

Mikutano hii hushirikisha waimbaji wa kwaya na vikundi mbalimbali  kwa kuwa nyimbo ni sehemu muhimu ya kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyokusudiwa,kumekuwa pia na utaratibu wa kuwa na wimbo mkuu wa mikutano hii,Miongoni mwa watu ambao wanaacha alama na kumbukumbu ya pekee ya utunzi wa nyimbo maalum za mikutano hii ni Mgini Kweba toka Tanzania.

HISTORIA
Mgini Kweba anaeleza kuwa alijiunga na kwaya ya SDA Magomeni Mwembechai jijini Dar es salaam September 16 ,1989 akiwa mwimbaji wa sauti ya tatu ambaye hakuwa na uzoefu wowote wa elimu ya muziki hata uimbaji. 

Anafafanua kuwa hakuwa na nia sana ya kuendelea kuwa mwimbaji kwa sababu alipendelea kusikiliza nyimbo zaidi ya kuimba. Hata hivyo, kuna mambo yalinimvutia kubaki kwenye kwenye kwaya, mojawapo ikiwa ni uimbaji wa ustadi kwa kufuata elimu ya muziki, urafiki wa waimbaji wenzake hasa sauti ya tatu ambao walikuwa ni, marehemu Richard Maira ambaye aliwahi kufundisha kwaya ya Mbeya na Kirumba wakati wa uhai wake, Jack Ndugu ambaye kwa sasa anaishi nchini Uingereza  na Abu Lukona.

"Zaidi sana nilivutiwa na ustadi na umahiri wa walimu wetu Kambira Mapesa na Gayo James  wakisaidiwa na marehemu Mshauri Blasius, marehemu Angelusha Alfred na Daniel Mwambene. Walimu hawa na waimbaji wa sauti ya tatu ndio walionipa msukumo wa kujifunza elimu ya muziki na ilipofika mwa 1993 nilikuwa tayari nimehitimu elimu ya msingi ya muziki iliyotosha kwangu kuanza kufundisha nyimbo."Anasema Mgini

UZOEFU:

Mwaka 1993-1995 alikuwa mwalimu msaidizi Magomeni SDA Choir 
1996-1998 - Mwalimu wa Kwaya Pasiansi SDA Mwanza 
1998-2000 - Mwalimu wa kwaya Njiro SDA Arusha


2000 – leo - Mwalimu wa kwaya Magomeni SDA Choir.
2004 – leo – Mwalimu na Mbia (partner) – TM Music Tanzania. 



UANDISHI WA NYIMBO:
Mgini Kweba anaeleza kuwa baada ya kuanza kuwa mwalimu, ufundishaji wake ulijikita katika kutafsiri nyimbo za watunzi mahiri duniani, jambo ambalo ndilo alirithi kutoka kwa walimu wake. 
Ilipofika  mwaka 2000,kutokana na ujio wa mtandao wa internet na matumizi zaidi ya computer yalimshawishi kujifunza matumizi ya teknolojia ili kuboresha ufundishaji wake

"Tangu wakati huo, nimesaidiwa na kuongeza kwa kiasi kikubwa elimu ya muziki kupitia teknolojia. Mwaka huo 2000, nilipokea ‘software’ ya kuandika muziki toka kwa Daniel Bulengela ambaye alikuwa mwalimu mwenzangu Pasiansi SDA Mwanza"anasema

Software hiyo ilikuwa ya majaribio (trial version) hivyo hakuweza kuitumia kwa matumizi yaliyokamilika. Hata hivyo mwaka mmoja baadaye mwalimu Mapesa Kambira ambaye aliwahi kuwa mwalimu wa Kwaya ya Magomeni  alihamia nchini Marekani na huko akamnunulia software iliyo kamili (full version) ambayo hadi leo anaitumia kuboresha kila wakati toleo jipya linapotolewa kwa kuwa yeye (Mgini) ni mmiliki halali. 

Kuanzia mwaka 2002 anaeleza kuwa  aliandika nyimbo za utunzi wake mwenyewe. Hadi leo zipo nyimbo nyingi ambazo ni utunzi wake zilizopo japo kuna ambazo hazijaimbwa na mtu hadi sasa, lakini anategemea zitaimbwa siku moja. Kwa ujumla, zipo pia nyimbo zaidi ya 200 alizokwishatafsiri kutoka kiingereza kwenda Kiswahili. Zipo chache alizoweza kutafsiri kutoka kijerumani kwenda Kiswahili kwa msaada wa tafsiri inayopatikana toka mtandao wa internet. 

UANDISHI WA NYIMBO ZA MIKUTANO: 

"Awali ya yote napenda kusema kuwa, kwa uzoefu wangu, mara kwa mara tukiwa na mikutano ya Kanisa na kuwa na wimbo wa mkutano, wimbo umekuwa ukipatikana kwa uchaguzi kutoka kitabu chetu cha nyimbo ‘Nyimbo za Kristo’. Tofauti niliyopata kukutana nayo ni katika mikutano ya makambi Magomeni, ambako kwa miaka miwili tofauti niliombwa kutafsiri nyimbo nyinginezo za Kikristo na kuimbwa kwenye kambi"Anasema Mgini

Mwalimu Mgini anafafanua kuwa Matumizi ya nyimbo za kutunga, maalum kwa mikutano, kwa kadri ya ufahamu wake ulianza mwaka  2018 wakati wa mikutano ya Maisha Hatimaye. Mchungaji Geoffrey Mbwana, mapema kabla ya mikutano kuanza, alifanya mawasiliano na Tumaini Murungu, mmojawapo ya waimbaji wa ‘Gospel Flames’ akiwataka watunge wimbo ambao ungehamasisha mkutano huo wa mjini Mbeya. Huu ndio ukawa mwanzo wa mtiririko ufuatao: 


Mkutano wa Maisha Hatimaye
Mgini anatabanaisha kuwa siku moja Jumapili asubuhi, takriban siku tano kabla ya mkutano wa Maisha Hatimaye kuanza, wakati akipata kifungua kinywa, alipokea simu toka kwa Tumaini Lameck aliyemwomba natunge wimbo kwa ajili ya mkutano wa ‘Maisha Hatimaye’ jijini Mbeya kama alivyokuwa ameombwa na Mch. Mbwana. Alimuuliza maudhui ya wimbo, akamwambia aandike tu kutokana na uzoefu wake kama Mkristo. 

Pale pale wakiongea, tayari sauti ya wimbo na mwendo wake vilianza kulia kichwani mwake. Alikubali kufanya kazi hiyo na moja kwa moja baada ya hapo alikwenda kwenye computer yake na kuanza kuandika kile alichokisikia kichwani. 

Anafafanua kuwa alipohitimisha kuandika sauti alijiuliza aandike maneno gani. Mawazo yake yakaenda kwenye Mathayo 6:25,33: Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? ...Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. 

"Kutokana na mafungu hay0, nilipata mawazo yaliyoniongoza kuweka maneno kwenye wimbo wangu nikizingatia muktadha wa mafungu hayo. Kesho yake baada ya masaa takribani 24 wimbo ulikuwa umekamilika kila kitu na nikamtumia Tumaini. 
Wimbo huu ukawa ndio wimbo mkuu wa mkutano"

Ufunuo wa Matumaini
Gospel Flames Quartet tena walielekea jijini Mwanza kwenye mkutano wa mchungaji Mark Finley wa ‘Ufunuo wa Matumaini’Mwalimu Mgini anaeleza kuwa Walimwomba tena kuwatungia wimbo wa ‘Ufunuo wa Matumaini’.
 Awali alisita kuwakubalia kwa sababu hakupenda aonekane tu kwa utunzi wa nyimbo za mikutano mikuu ila baada ya ushawishi mwingi hatimaye alikubali. 

Alitunga wimbo wa “Ufunuo wa Matumaini’ ambao japo haukuwa ndio wimbo mkuu, waliuimba huko na baadaye wakauimba kama wimbo wa mkutano wa injili wa ‘Medali ya Matumaini’ uliofanyika Eldoret Kenya, uliohubiriwa na Mch Geoffrey Mbwana 

Nyumbani Hatimaye.
Mgini Kweba anaishi  Kinyerezi Dar es salaam japo ni mshiriki wa Magomeni. Nyakati nyingine huwa anasali Kanisa la Waadventista wa Sabato  Kinyerezi na mojawapo ya nyakati hizo ndipo alikutana na Kikundi cha Mtende na wakamwomba awafundishe nyimbo. Alikubali na sasa, kwa takriban miaka miwili amekuwa mwalimu wao na ameshawafundisha nyimbo zaidi ya 24. 

Anaeleza kuwa alikubali kuwa mwalimu wao baada ya kutambua kipaji cha pekee walicho nacho kiuimbaji. Waanzilishi wa kikundi ni watu wanne, mmoja mmoja kila sauti, ila aliwashauri  waongeze watu ikiwezekana kuwa wawili wawili kila sauti ili inapotokea dharura mmojawapo hayupo bado uimbaji uendelee. Kwa sababu hiyo, kwa sasa wamefikia watu 7. 

"Rafiki zangu wa Mtende walitambua kuwa nilikuwa mtunzi wa wimbo wa mkutano wa Mbeya na kwa kuwa sasa Kanisa lao ndilo lilitazamiwa kuwa wenyeji wa mkutano wa Nyumbani Hatimaye, wao pia wakapata hamu ya kutoa mchango wao kwa wimbo mkuu wa mkutano na wakaniomba niwatungie wimbo"Anasema

"Wakati huu nilisita zaidi na nikawatahadharisha kuwa haikuwa lazima wao ndio waimbe wimbo mkuu, wakasema walikuwa na hiari kwa hilo pia ila wakanisihi niendelee. Nilikubali na hapo ndipo wimbo wa Nyumbani Hatimaye ulipozaliwa"

Anasema kama ilivyokuwa kwa nyimbo zilizotangulia, hakuwa na maudhui ya mkutano zaidi ya kichwa cha habari tu na akafanya tafsiri binafsi neno hili lina maana gani kwake. Alifungua Biblia yake na akapata msaada wa mafungu yafuatayo kupata maneno ya wimbo: 


1. Yohana 14:1-3: “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe wangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo”. 

2. Wafilipi 3:20 “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo” 

3. Tito 2:13 “Tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu” 

Baada ya kutunga wimbo huu, Mtende walijifunza kwa uaminifu kisha kuurekodi na wameshuhudiwa  wakiimba baada ya kuuwasilisha kwa kamati ya maandalizi pamoja na muziki wake wa kuandikwa, mwisho ukapitishwa na kuimbwa ukiwa ni wimbo wa Mkutano wa Nyumbani Hatimaye 2019

Mgini anamaliza makala hii kwa kueleza kuwa jambo la msingi la kuelewa pia ni kuwa kazi zote hizi nimezifanya kwa kujitolea. Hakuna malipo yoyote aliyopokea kulipia kazi yake.Huyu ndiye Mgini Kweba 





1 comment

Anonymous said...

Ubarikiwe mwalimu kwa kujitolea kufanya kazi ya Mungu. Taji yako ipo mbinguni.

Mtazamo News . Powered by Blogger.