MPANGO WA UENDESHAJI WA KIJINSIA KWA AJILI YA MWITIKIO WA UKIMWI TANZANIA BARA
Mratibu wa Jinsia kutoka TACAIDS Jacob Kayombo na Afisa Jinsia kutoka TACAIDS Judith Luande wakijadili baadhi ya maoni, maswali na mapendekezo ya wajumbe ambao ni timu ya kudhibiti Ukimwi ya Mkoa wa Singida wakati wa Mafunzo juu ya mpango wa uendeshaji wa kijinsia.
Mjumbe wa mafunzo juu ya mpango wa uendeshaji wa kijinsia Afisa wa Serikali za Mitaa Hussein Mwatawala akipitia fomu zitakazotumika katika kukusanya taarifa za masuala ya Kijinsia mkoani Singida.
Serikali ya Tanzana kupitia Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) imeandaa Mpango wa uendeshaji wa Kijinsia kwa ajili ya mwitikio wa Masuala ya Ukimwi ambao umetambulishwa rasmi kwa timu ya Kuthibiti Ukimwi Mkoani Singida.
Mratibu wa Jinsia Kutoka TACAIDS Jacob Kayombo ameongoza mafunzo hayo kwa timu ya kuthibiti Ukimwi Mkoa wa Singida ambapo amewaeleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuratibu na kutoa dira katika utekelezaji wa program mbalimbali za Ukimwi kwa ngazi ya Mkoa.
Kayombo amesema Mafunzo hayo yamelenga kuutambulisha mpango huo pamoja na fomu zitakazotumika katika ukusanyaji wa taarifa zihusuzo jinsia na Ukimwi.
Kayombo amesisitiza kuwa mpango huu utakuwa ni mwongozo wa wadau wa masuala ya Ukimwi ili waweze kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia usawa wa kijinsia hasa katika kuweka mikakati ya kuthibiti Ukimwi yenye uelekeo wa Usawa wa kijinsia.
Amebainisha kuwa mpango huu ambao umedumu katika kipindi cha mwaka 2016 mpaka 2018 una mwelekeo mpya wa program za ukimwi wenye kuzingatia masuala ya kijinsia pamoja na kuondoa changamoto zitokanazo na mila na desturi potofu za masuala ya kijinsia.
Naye Mjumbe wa mafunzo hayo Afisa wa Serikali za Mitaa Hussein Mwatawala amesema mafunzo hayo yametoa mwanga na mwelekeo utakawaosaidia katika kusimamia wadau wanaotekeleza shughuliza Ukimwi ili wazingatie usawa wa kijinsia mkoani hapa.
Mwatawala amesema maafisa waliopata mafunzo hayo wamepewa elimu ya kutosha juu ya mpango na wameufahamu vema kazi iliyobaki ni kuhakikisha masuala ya usawa ya kijinsia yanapewa kipaumbele katika kila program ya Ukimwi inayotekelezwa na wadau mkoani hapa.
Mpango wa uendeshaji wa masuala ya Kijinsia 2016-2018 umeanzishwa kwa lengo la kutoa mwongozo kwa wadau wa masuala ya Ukimwi ili watekeleze program zao katika mtazamo wa usawa wa kijinsia.
Mpango huu unashughulikia tofauti za kijinsia zikiwemo ukatili wa kijinsia, unyanyapaa na ubaguzi ili kulinda haki za watu wote wakiwemo wanaume,wanawake,wasichana na wavulana ili wapate huduma za uzuiaji wa maambukizi ya VVU, tiba, matunzo na msaada.
Mpango huu unahusianishwa na Mkakati wa tatu wa taifa wa kuthibiti Ukimwi 2013-2018 na Mkakati wa tatu wa kuthibiti VVU na Ukimwi wa Sekta ya Afya 2013-2017 ambapo mikakati hiyo ina kanuni ambazo zinajumuisha usawa wa kijinsia na ulinzi wa haki za binadamu.
Post a Comment