MTANGAZAJI

DC WILAYA YA NYANG'WALE AELEZA ATHALI ZA UKOSEFU WA CHAKULA


 Mkuu wa Wilaya ya Nyang'wale Mkoa wa Geita,  Hamim Buzohera Gwiyama (katikati), akizungumza na watafiti wa kilimo kutoka  Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Ukiriguru Mwanza, Ilonga mkoani Morogoro na Waandishi wa Habari kabla ya kukabidhiwa mbegu bora za mahindi na mhogo kwa ajili ya kuzipanda kwenye mashamba darasa katika vijiji vinne wilayani humo. Kulia ni Diwani wa Kata ya Nyugwa, Ndozi Manual na kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Fabian Sospeter ambaye alikabidhiwa mbegu hizo na kuhutubia wananchi kwa niaba ya mkuu huyo wa wilaya.

 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi, akimkabidhi mbegu ya mhogo aina ya Mkombozi Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Fabian Sospeter kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo.

.
 Mkulima Pendo Sangoma akishiriki kupanda mbegu ya Wema katika shamba darasa katika Kijiji cha Kakora wilaya humo. Kushoto ni Ofisa Ugani, David Makabila kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang'wale Mkoa wa Geita Hamim Buzohera Gwiyama amesema bila ya kuwepo kwa usalama wa chakula nchini bado kutaendelea kuwepo na changamoto nyingi za maendeleo na kuwa pasipo chakula hakuna kitakachoweza kufanyika.

Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Fabian Sospeter  kwa niaba ya Mkuu huyo wa wilaya hiyo, Hamim Gwiyana amesema  jana wakati akipokea mbegu bora za mahindi aina ya Wema na mhogo aina ya Mkombozi kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) kwa ajili ya kuanzisha mashamba darasa ya mbegu katika vijiji vya Kakora, Nyang'wale, Kanegele na Nyugwa.

Alisema usalama wa kujilinda na adui hauna shida kwani mtu anaweza kuandaa jeshi lake la kukabiliana na adui huku akiwa na silaha nzito lakini sio usalama wa chakula ambao unahitaji maandalizi ya kutosha na watu kujituma na kufanya kazi kwa bidii hasa za kilimo chenye tija.

Alisema kukosekana kwa chakula mara nyingi kunachangiwa na tabia za baadhi ya watu kuharibu mazingira kwa kukata miti hovyo hivyo kusababisha mvua kushindwa kunyesha  na maeneo mengi kuwa na ukame.

Alisema katika wilaya yake njaa imechangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kuwa watoro na kushindwa kumaliza shule na kuwa kukosekana kwa chakula kwa watu ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, alisema kuwa kazi kubwa ya COSTECH ni kuishauri serikali katika masuala yote yanayohusu  Sayansi na Teknolojia na kusimamia tafiti zote za kisayansi katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha matunda ya tafiti hizo yanawafikia walengwa.

Alisema mbegu hizo walizozikabidhi ikiwamo ya mahindi yanayostahimili ukame ya Wema 2109 na mhogo zimefanyiwa utafiti na zitapandwa katika mashamba darasa na baadae kusambazwa kwa wakulima wengine ili kuondoa changamoto ya kukosekana kwa mbegu bora kutokana na wakulima kukabiliwa na mbegu ambazo zilikuwa na magonjwa. 

Dk. Bakari aliwataka wakulima na maofisa ugani kuyatunza mashamba darasa hayo ili kazi kubwa iliyofanyika isipotee bure na baada ya muda mfupi watarudi kuangalia maendeleo yake.
Na Dotto Mwaibale


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.