MTANGAZAJI

MAMBO 10 ANAYOTAKIWA KUWA NAYO MWANAUME KATIKA UMRI WA MIAKA 30


Watanzania wana misemo mingi inayoendana na umri lengo likiwa ni kukumbushana katika kuwajibika na kujipanga katika maisha ya kawaida. Miongoni mwa misemo hiyo ni, ‘Ujana maji ya moto, fainali uzeeni.’ Msemo huu una maana kubwa kama ukiutafakari kwa makini, lakini kwa tafsiri ya haraka ni kwamba ujana ndio kipindi ambacho mtu huwa na nguvu za kutosha kufanya masuala tofauti yatakayomuwezesha kuishi vema uzeeni. Licha ya kuwa na nguvu hizo lakini huwa na changamoto kadhaa zinazomuandama ambapo kama asipokuwa makini atakuja kujuta akiwa uzeeni.
Mojawapo ya changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi ni kutokujua vitu gani vya kuweka kipaumbele katika wakati waliopo. Kulingana na umri waliokuwa nao huona kwamba muda unawatosha na hivyo kufanya masuala yasiyo na tija wala kujijengea misingi mizuri ya kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye. Kwa kuliona hilo, Jumia Travel imeona ni vema kukushirikisha wewe kama kijana wa kiume ni mambo gani ya msingi unatakiwa kuwa nayo ukiwa katika umri wa miaka 30.
  
Kupevuka kiakili. Ingawa suala la kupevuka kwa akili halihusiani na umri lakini kufikia umri wa miaka 30 kama mwanaume unatakiwa kuonyesha ukomavu wa akili wa hali ya juu. Hili huweza kupimwa kutokana na misimamo uliyonayo na uwezo wa kufanya maamuzi juu ya masuala mbalimbali yanayoathiri maisha yako. Maisha hutofautiana kwani kuna wengine hupevuka kiakili wakiwa katika umri mdogo na wengine huwachukua muda. Kwa mfano, katika umri huu kushindwa kujua ni nini unakitaka katika maisha yako kinaweza kuibua wasiwasi kwa wazazi, ndugu au jamii nzima inayokuzunguka. 
Kuwa katika mahusiano ya kudumu. Kuna ule usemi unaosema, ‘Vunja mifupa kama meno bado ipo,’ ulijipatia umaarufu pia kupitia mwanamuziki mashuhuri wa muziki wa bolingo, Samba Mapangala. Semi huwa zina maana tofauti kulingana na watu wataamua kuzitafsiri na kuzitumia kwa malengo gani. Lakini itapendeza kuzitumia katika njia zenye manufaa zaidi. Vijana wengi huubeba usemi huo na kuutafsiri kama ukiwa kijana pengine huwa ni fursa ya kujihusisha na mahusiano na wanawake tofauti tena kwa nyakati tofauti. Lengo, eti, ni kupata uzoefu na kupata mambo ya kuhadithia enzi za ujana wako zilikuwaje pindi uzeekapo. Kama unafanya hivyo unajiongopea. Kuwa na mahusiano ya kudumu na msichana mmoja hukupatia fursa mwanaume ya kutulia na kujipanga na maisha yako.    
Kuelimika (darasani au njia nyinginezo). Zipo njia nyingi za kujielimisha sio lazima mpaka upitie darasani na kupata astashahada, stashahada au shahada juu ya taaluma mbalimbali. Vipato na fursa hutofautiana katika kulifanikisha hilo, lakini kama unapata fursa hiyo ni vema kuitumia ipasavyo. Elimu pia hupatikana kwa njia ya mafunzo, semina, warsha au kufundishwa na watu wa kawaida ambapo fursa ni nyingi katika jamii inayokuzunguka. Zipo fursa za kujifunza katika jamii tunamoishi lakini watu hupuuzia tena zingine huwa ni bure kabisa. Mwanaume katika umri wa miaka 30 hakikisha unakuwa na elimu, ujuzi au ufahamu juu ya mambo tofauti ambayo yatakurahisishia katika kupata kipato kwa urahisi.
Kuwa na makazi maalum au ya kudumu. Siyo lazima mpaka ujenge kwani hilo linategemeana na uwezo wa mtu lakini unaweza kupanga pia. Itakuwa ni vema katika umri huu mwanaume unakuwa unaishi kwako. Hii itakurahisishia zaidi kujipanga zaidi katika maisha yako. Ingawa kuna familia zingine huwa zina namna tofauti za kuwaruhusu vijana wao kujitegemea lakini hata kama mnamiliki nyumba kubwa au kadhaa za kuishi basi angalau unakuwa na sehemu yako ukijtegemea. 
Kuwa na shughuli ya kujiingizia kipato (kuajiriwa au kujiajiri). Katika jamii yoyote ile hatutegemei kumuona kijana wa umri wa miaka 30 bado akiwa yupo nyumbani hajishughulishi na shughuli yoyote ya kujiingizia kipato. Sio lazima mpaka uajiriwe ila kama una fursa hiyo ni vizuri lakini pia unaweza kujiajiri kwa kufanya biashara zako mwenyewe.

Kujitegemea. Kwa familia zetu za kiafrika hususani kitanzania kuna umri ukifikia wazazi huwa hawajihusishi kabisa na wewe kwa kukuhudumia. Jitihada zote huelekezwa kwa wengine wadogo na tena huhitajika wewe kama mkubwa kuwasaidia kwa masuala madogomadogo. Itakuwa ni jambo la aibu kwa mwanaume wa miaka 30 analalamika eti hapewi hela ya matumizi na wazazi wake au ananyimwa fedha za kununulia hata mavazi yake mwenyewe. 
Kuwajibika. Kuna mambo fulani kama vijana huwa tunayafanya kwa kujiamini kwamba umri una ruhusu na muda upo wa kutosha wa kuja kutulia siku za usoni. Lakini katika umri wa miaka 30 inabidi sasa ubadilike kwa kuachana na baadhi tabia ambazo unaona hazikusaidii katika maisha yako ya sasa na baadaye. Inabidi ufikie muda sasa uanze kuwajibika kwako wewe mwenyewe na watu wako wa karibu wanaokuzunguka.  

Kujiwekea malengo. Kama unamfuatilia mwanzilishi wa kampuni ya Alibaba ambayo inajihusisha na manunuzi kwa njia ya mtandao duniani, Bw. Jack Ma, basi utakuwa umekumbana na msemo wake unaosema, ‘Ukiwa masikini katika umri wa miaka 35 basi utakuwa umejitakia mwenyewe.’ Msemo huu una maana kubwa sana katika kutukumbusha kwamba ili kufanikiwa katika maisha lazima tujiwekee malengo na mikakati ya namna ya kuyafanikisha. Kama kijana kamwe usitarajie miujiza ya mafanikio kama unaishi bila ya kujiwekea malengo. Haijalishi iwe ni ya mwaka mmoja, mitano au kumi, ni vema kujiwekea na kuwekeza bidii na jitihada katika kuhakikisha unayafanikisha. 

Kujua kuendesha chombo cha moto (gari au pikipiki). Kuna msemo maarufu wa wazungu unaosema, ‘Mafanikio huja pale maandalizi yanapokutana na fursa.’ Nadhani utakuwa umekwisha kukutana na simulizi za mtu kukosa kazi kwa sababu tu ya kutokuwa na ujuzi fulani. Katika dunia ya sasa miongoni mwa ujuzi ambao mtu anatakiwa kuwa nao ni udereva wa chombo cha moto iwe ni pikipiki au gari. Kwanza ni rahisi kujifunza, pili vyuo vipo vingi vya kujinza na tatu haihitaji gharama kubwa kufanya hivyo. Kuwa na ujuzi huu ni faida kubwa kwa mwajiri kwani pengine inaweza kumrahisishia gharama za kumuajiri na kumlipa mtu mwingine kufanya hivyo.   

Kujiwekea akiba. Kama kijana lazima uwe na mpango wa kujiwekea akiba sasa kwa ajili ya maisha yako ya baadaye. Zipo njia nyingi za kuweka akiba kwa sasa zinazotolewa na taasisi mbalimbali ukiachana na ile ya lazima ambayo serikali huwataka waajiri kuwaunganisha wafanyakazi wao na mifuko ya hifadhi za kijamii. Kama kijana pia unaweza kufanya hivyo kwa kutembelea benki na mifuko tofauti na kujua ni namna gani unaweza kufanya hivyo.

Nafikiri utakuwa umejifunza au angalau kufunguka akili juu ya masuala ya msingi ya kuyazingatia kama kijana unayeingia au tayari una umri wa miaka 30. Kama bado haujafanya au kufanikikisha jambo lolote miongoni mwa yaliyotajwa hapa, Jumia Travel inaamini bado haujachelewa. Fanya maamuzi na ujipange sasa ili kuwa kijana mfano wa kuigwa kwa jamii na taifa kwa ujumla. 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.