MTANGAZAJI

UJUMBE WA WAKAZI WANAOPAKANA NA MBUGA YA SERENGETI WAPANGA KUONANA NA RAIS KIKWETEMchakato wa kuwahamisha  wakazi wapatao 8112 wa vijiji vitatu vya Serengeti, Nyatwali na Tamau vya wilayani Bunda umeingia sura mpya baada ya wakazi wa vijiji hivyo kuunda ujumbe wa watu sita kwenda kumwona rais Kikwete.

Ujumbe huo unaojumuisha wazee watatu na wenyeviti wa serikali za vijiji hivyo unatarajia kuondoka mjini bunda mwishoni mwa juma kuelekea jijini Dar es Salaam tayari kuwasilisha kilio chao kwa mkuu huyo wa nchi.

Wakiongea na waandishi wa habari waliotembelea vijiji hivyo juzi wakazi hao wamesema wameamua kutuma ujumbe maalum kwa rais baada ya kubaini kuwa zoezi la kuwahamisha halina baraka za serikali kuu.

Walisema tangu zoezi hilo lianze mapema mwaka huu wahusika wameshindwa kuwasilisha nyaraka zinazotengua sheria iliyovitenga kama vijiji halali miaka takribani 60 iliyopita vikitambulika kama majirani wa hifadhi hiyo.

Wakazi hao wa vijiji hivyo vilivyoko kandokando ya ziwa Victoria vikipakana na hifadhi ya taifa ya Serengeti vinatakiwa kuhamishwa ili kupisha eneo hilo liwe sehemu ya hifadhi hiyo yenye kujaa na vivutio vya kila aina vya utalii.

Kwa kufanya hivyo kutawawezesha wanyama walioko katika hifadhi hiyo kunywa maji kutoka ziwa hilo kufuatia kuwepo kwa upungufu wa maji ndani ya hifadhi hiyo ulioletelezwa na kukauka kwa mito iliyokuwa ikitegemewa.

Uamuzi huo wa wakazi hao kutuma ujumbe kwa rais unakuja siku chache baada ya kamati ya ushauri ya wilaya hiyo kuridhia wakazi hao wahame huku wao kwa nyakati tofauti wakisisitizia kutofanya hivyo mpaka wasikie kauli ya Rais Kikwete.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.