MTANGAZAJI

BARAZA LA MADIWANI TARIME LATAKA WAZAZI WASIOPELEKA WATOTO SHULE WASHITAKIWEBaraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime limepitisha azimio la kuwafikisha mahakamani wazazi ambao hawawajibiki ipasavyo kuwapeleka watoto waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu ili kujibu tuhuma za kutotekeleza jukumu hilo baada ya wakuu wa shule za sekondari kuyabaini majina ya wanafunzi watoro.

Azimio hilo limefikiwa katika kikao cha baraza la madiwani kinachofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambapo wamemtaka Mkurugenzi Mtendaji Athuman Akalama kushughulikia tatizo hilo haraka ili kuboresha kiwango cha elimu kinachoelezwa kushuka wilayani humo.

Diwani wa kata ya Pemba Paradiso Mogesi amesema kuwa katika kata yake asilimia 21 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka  2014 hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa kujiunga.

Amesema kuwa ili kukomesha tabia hiyo ya baadhi ya wazazi wasioona umuhimu wa kuwapeleka watoto wao shule katika vikao toka ngazi ya vijiji na mkutano mkuu wa kata, wamewaagiza wakuu wa shule za sekondari katika kata yake kuwaorodhesha wanafunzi wote ili kubaini wanafunzi watoro na kuanza kuwashughulikia wazazi wao.

Afisa utumishi wa Halmashauri hiyo Bakaran Urio   akionesha kuguswa na hali hiyo amewataka viongozi  husika kulifikisha tatizo hilo ofisini kwake ili kulishughulikia haraka iwezekanavyo.No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.