MTANGAZAJI

VIJANA WA KANISA LA WAADVENTISTA WA SABATO MWANZA WACHANGIA DAMU

Idara ya Vijana Kanisa la Waadventista Wa Sabato Kanda ya Mwanza Mashariki, wamechangia jumla ya mililita 36,750 za damu katika Benki ya damu salama.

Jumla ya vijana 105 kutoka katika makanisa 25 ya Kanda hiyo ya Mashariki mwa jiji la Mwanza, walikusanyika Jumamosi iliyopita katika Kanisa la Waadventista wa Sabato Igoma, ili kuchangia damu katika Benki ya Damu salama.


Naye Mratibu wa Vijana wa Kiadventista wa Kisabato Kanda ya Mashariki mwa Jiji la Mwanza,David Kitundu, ameiambia Radio Morning Star FM kwamba vijana hao 105 walichangia damu kiasi cha mililita 36,750 zilizotokana na jumla ya chupa 105 zenye ujazo wa mililita 350 kila moja.


Mratibu huyo wa vijana Mashariki mwa Jiji la Mwanza,David Kitundu, ameitaja mitaa iliyoshiriki kutoa damu hiyo kuwa ni Nyanguge, Shamariwa, Igoma,Nyakato na Buzuruga yote ya jijini humo.

Kwa upande wake afisa Utawala wa Benki ya Damu salama ,Innocent Biabesa, amesema hitaji la damu salama kwa mwaka jijini Mwanza, ni lita 100,000; na kwamba kila mwaka Mwanza kuna upungufu wa damu wa kati ya lita 25,000 na 30,000.


Utoaji damu kwa hiari uliofanywa na vijana hao wa Waadventista Wa Sabato katika siku ya Matendo ya Huruma Duniani,Machi 15 mwaka huu,umekuja Mwanza kukiwa na madai ya Matabibu na Wauguzi wa hospitali kuwauzia wagonjwa chupa moja ya damu kwa shilingi laki tatu.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.