MWENYEKITI WA KIJIJI ATAKA KUJIUZULU KWA SABABU YA MWEKEZAJI
Mgogoro wa shamba unaoendelea kati ya mmiliki mwenye asili ya
kiasia Pradeepo Lodhia wa shamba la Tanzania Plantation na wananchi wa
kijiji cha Msitu wa Mbogo kata ya Mbuguni wilayani Arumeru mkoani
Arusha umechukua sura mpya baada ya mwenyekiti wa kijiji hicho Ernesti
Mkilanya kutangaza kujiuzulu wadhifa wake iwapo wananchi wanaoendelea na
uvamizi katika shamba la mwekezaji huyo hawataacha mara moja.
Mwenyekiti wa kijiji huyo ameyasema hayo mapema wiki hii wakati akizungumza na wananchi wa kijiji
hicho na kuwataka wananchi kuwataja na kuwafichua wote wanaohusika kwa
njia yoyote ile kuhujumu shamba la
mwekezaji huyo mara moja.
Mwenyekiti huyo ameyasema hayo wakati mgogoro huo ukiwa umedumu
kwa takribani miezi mitatu sasa
Wito huo umekuja wakati
viongozi wa kijiji hicho wakiwa wamepokea barua ya onyo ya kumbukumbu
namba 201 ESM inayotoka kwa wakili wa mwekezaji huyo Loamu Ojari
inayotaka viongozi wa kijiji hicho wasitishe uvamizi na uharibifu wa
mali katika shamba hilo vinginevyo watashitakiwa.
Hivyo
Bwana Mkilanya amesema atajiuzulu ili kupisha wengine kugombea nafasi
hiyo kwani hawezi kushitakiwa mahakamani kwa tuhuma za uvamizi wa shamba
hilo wakati yeye pamoja na viongozi wengine wa kijiji hawahusiki na
chochote.
Aidha bwana Mkilanya alisema kuwa kamati ya ardhi yenye wajumbe
25 iliundwa february 5 mwaka huu na imeshafikisha malalamiko hayo kwa
mkuu wa wilaya ya Arumeru ambapo ameahidi kulishughulikia.
Na:Abeli Kinyongo
Post a Comment