MTANGAZAJI

KIKOSI KAZI CHA KUKOMESHA MAUAJI YA WAZEE NCHINI TANZANIA CHAUNDWA NA WAZIRI NCHIMBI

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi ameunda Kikosi Kazi kitakachokuwa na jukumu la Kuratibu  na Kusimamia Ukomeshwaji wa Vitendo vya mauaji ya Wazee, yanayotokea mara kwa mara katika maeneo ya  Kanda ya Ziwa hapa nchini.
Kuundwa kwa Kikosi Kazi hicho kunatokana na kukithiri kwa ongezeko la matukio ya mauaji ya wazee, yanayotokana na imani za kishirikina yanayotokea  katika baadhi ya Mikoa ya Tanzania Bara hususani Kanda ya Ziwa ambayo yamekuwa yakisababisha madhara makubwa katika jamii ya Watanzania. 

Miongoni mwa madhara hayo ni pamoja na Watu kufariki dunia hususani wazee, Matukio hayo kuendelea kuacha makovu 

ya chuki  na hisia  za kulipiza kisasi, Matumizi  ya ziada ya rasilimali  katika kuimarisha miundo mbinu  ya ulinzi na usalama, ikiwemo pia Nchi kupoteza sifa  ya kuwa kisiwa cha amani.
Kikosi Kazi hicho chenye wajumbe kumi (10) ambacho kimeanza kazi tangu  Oktoba Mosi mwaka huu kinaongozwa na Mwenyekiti wake Naibu Kamishna wa Polisi Ernest Mangu ambaye pia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza.

Wajumbe wengine wa Kikosi Kazi hicho ni pamoja na Kamishna Msaidizi wa Polisi Leornard Paul ambaye ni  Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita,Kamishna Msaidizi wa Polisi Salum Msangi ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu,Kamishna Msaidizi wa Polisi Peter Ouma ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora.

Wajumbe wengine kutoka vyombo vya ulinzi na usalama ni  pamoja na Jacob Mutashongerwa, Gaston Peter Ndwata, Fulcon Nguli, Roman Matemu, na Anna Tegullo.

Hatua ya kuundwa kwa Kikosi Kazi hicho, kitakachofanya kazi kwa muda wa miezi sita ni Mkakati wa Serikali kupitia Jeshi la Polisi kushughulikia ukomeshwaji  wa tatizo la mauaji ya wazee yanayotokea hasa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu na Tabora.

Lengo la kuundwa kwa Kikosi Kazi hicho ni kutafuta njia mbadala za kukomesha mifumo  ya kijamii inayoweka  imani za kishirikina zinazosababisha  mauaji katika umri wa wazee ambao wanahitaji kuishi kama raia wengine.

Kikosi kazi hiki kitakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa njia zitakazotumika kukomesha mifumo ya kijamii inayochangia kasi ya kuongezeka kwa mauaji ya wazee zinabadilisha mtazamo hasi wa jamii ambayo badala ya kuwaenzi wazee imegeuka kwa kuwatuhumu kuwa ni watu wabaya na hawafai kuishi na hatimaye kuwaua kikatili kwa visingizio vya imani za kishirikina.

Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI,
11Oktoba, 2013

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.