MTANGAZAJI

RAIS KIKWETE NA RAIS KAGAME WAKUTANA KWA FARAGHA NCHINI UGANDA

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , Alhamisi, Septemba 5, 2013, amekutana kwa faragha na Rais wa Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame katika mazungumzo yaliyokwenda vizuri na kuwaridhisha viongozi hao wawili wa nchi jirani.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Septemba 5, na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu ya Tanzania imeeleza kuwa Viongozi hao wamekutana kwa zaidi  ya saa moja katika mkutano uliofanyika kwenye Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, nje kidogo ya mji wa Kampala, Uganda.

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete na Rais Kagame wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika kujenga 

uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Viongozi hao wawili wako nchini Uganda kuhudhuria Mkutano wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Kimataifa wa Maziwa Makuu – “International Conference on the Great Lakes Region (ICGLR)” unaofanyika leo Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort.

Viongozi wengine ambao wanahudhuria Mkutano huo ni pamoja na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa ICGLR na mwenyeji wa Mkutano huo, Rais Silva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).

Rais Kikwete na ujumbe wake waliwasili  Kampala asubuhi ya jana akitokea mjini Dodoma ambako aliwasili juzi jioni kwa ajili ya hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu watatu na Naibu Makatibu Wakuuu wawili iliyofanyika Ikulu Ndogo, Dodoma.

Rais Kikwete aliwasili Dodoma akitokea Mwanza ambako alihudhuria mazishi ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Askofu Mkuu Dkt. Moses Samwel Kulola yaliyofanyika kwenye Kanisa la Bugando Calvary Temple, mjini Mwanza.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.