MTANGAZAJI

LEO SIKU YA WAANDISHI WA HABARI DUNIANI

Waandishi wa habari Tanzania wanaungana na waandishi wenzao duniani kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo Habari, ambayo kitaifa inafanyika jijini hapa leo.

Tofauti na miaka mingine, taasisi mbalimbali za waandishi wa habari zimeungana kwa pamoja kuadhimisha siku hiyo ambapo mada kuu ya maadhimisho hayo ni Usalama na mazingira bora ya kufanyia kazi kwa waandishi wa habari.


Mkurugenzi wa Taifa wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tanzania (Misa-Tanzania), Tumaini Mwailenge, alisema kumekuwa na hali inayotishia utendaji kazi kwa waandishi wengi wa habari, suala ambalo haliwezi kufumbiwa macho.


Alitaja  waandishi wa habari waliotendewa unyama kutokana na kazi zao kama kuuawa kwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel 10, Daud Mwangosi, kumwagiwa tindikali na kupigwa kwa Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage na tukio la hivi karibuni la Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda, kuwa ni baadhi tu ya mifano ya waandishi wa habari wachache waliokumbana na ukatili dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini.


Hata hivyo, alisema wapo waandishi wa habari wengi ambao wanaendelea kupokea vitisho vya kufanyiwa unyama kutokana na kazi zao.


Mada zingine zitakazotolewa ni kuhusu suala la Ualama wa Vyombo vya Habari, Mabadiliko ya Vyombo vya Habari na Haki za Binadamu pamoja na changamoto zake zinatarajiwa kutolewa.


Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Umoja wa Vilabu wa Waandishi wa Habari Tanzania, Jane Mihanji, na Katibu wa Jukawaa la Wahariri Tanzania, Neville Meena, waliwataka waandishi wa habari kuwa na umoja, kupendana na kushirikiana katika kazi zao.


Mwandishi Mwandamizi kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT), Allan Lawa alisema alitoa ufafanuzi kuhusu siku ya uhuru wa habari akisema hauna lengo la kugombana na serikali isipokuwa kueleza masuala yanayowasibu ili jamii na serikali ipate kusikia na kuyafanyia kazi.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.