VITAMBULISHO VYA TAIFA NCHINI TANZANIA KUANZA KUTOLEWA FEBRUARI 7,2013
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akitia saini ya kitambusho cha Taifa |
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa nchini (NIDA)
imemweleza Rais Jakaya Kikwete kuwa Vitambulisho vya Taifa vinatarajia
kuanza kutolewa rasmi Februari 7, 2013. Taarifa hiyo imetolewa jijini
Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA), Dickson Maimu wakati Mkurugenzi huyo na ujumbe wake walipofika
nyumbani kwa rais kukamilisha taratibu za uandikishaji wa kitambulisho
chake.
Kwenye tukio hilo la muda mfupi na lililoshuhudiwa pia na Mama Salma
Kikwete, Rais Kikwete ametakiwa kuthibitisha ukweli wa habari
zilizojazwa kwenye fomu yake ya uandikishaji, akapiga picha rasmi ya
kitambulisho chake na kutiwa saini kwenye kitambulisho chake
anachondaliwa na NIDA.
Maimu amemwambia Rais Kikwete kuwa wakati wa uzinduzi huo wa utoaji
Vitambulisho vya Taifa utakaofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es
Salaam, NIDA itatoa vitambulisho kwa viongozi wakuu wa taifa na
viongozi wakuu wastaafu.
Amesema kuwa baada ya sherehe hizo ya uzinduzi wa utoaji Vitambulisho
vya Taifa, maofisa wa NIDA watatoa Vitambulisho kwa Wabunge na Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Maimu pia amemwambia Rais Kikwete
kuwa inakadiriwa kuwa kiasi cha Watanzania milioni 21, wenye umri wa
zaidi ya miaka 18, watajiandikisha kwa ajili ya kupatiwa Vitambulisho na
kuwa orodha hiyo itaweza kutumiwa na taasisi nyingine nchini ikiwa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi na mabenki.
Rais Kikwete pia alitaka kujua nchi nyingine zinaendesha vipi suala
zima la vitambulisho hasa kuhusiana na kuvitoa bure kwa wananchi na
Maimu amesema kuwa kwa Tanzania gharama za Vitambulisho vya Taifa
zitabebwa na taasisi ambazo zitatumia habari na takwimu zilizoandaliwa
na NIDA.
Rais Kikwete ameishukuru mno NIDA kwa hatua zilizofikia kuelekea
kupatikana kwa Vitambulicho vya Taifa. “Nawashukuru sana kwa kufikia
hatua ya sasa. Tumeanza mbali mno na suala hilo, tokea mwaka 1968.
Nafurahi sana kuwa tumefikia mahali pa kuweza kutoa Vitambulisho vya
Taifa.”
NIDA ilianza zoezi la kuandikisha wananchi kwa ajili ya kutoa
Vitambulivyo vya Taifa mwishoni mwa mwaka 2011 baada ya kukamilisha
zoezi zima la maandalizi ya kuifanya kazi hiyo.
Chanzo:The Habari.com
Post a Comment