MTANGAZAJI

SIMULIZI TOKA KWA KAKA MJENGWA-WAZEE WA DAR ES SALAAM NI AKINA NANI?

Ndugu zangu,

TANGU ‘Enzi za Mwalimu’, kukiwa na jambo kubwa kitaifa, basi, Mwalimu aliliongea kupitia kwa “ Wazee Wa Dar Es Salaam”. Na mahali haswa wanapokutana ‘Wazee wa Jiji’ kumsikiliza ‘ Mkuu Wa Kaya’ ni pale Upanga kwenye Ukumbi wa Diamond.


Jambo hilo lililoasisiwa na Mwalimu sasa limekuwa ni utamaduni wa kisiasa. Mathalan, ni pale Upanga Diamond Jubilee ndipo Mwalimu alipotangaza vita dhidi ya Idi Amin kupitia Wazee Wa Dar Es Salaam . Nilipokuwa mtoto pale Ilala, nilitamani sana nikue nije kuwa mtu mzima, kisha niwe mmoja wa ‘ Wazee wa Dar Es Salaam’ ! Ndoto yangu hiyo imefutika! Naam, nimepoteza sifa ya kuwa ‘ Mzee wa Dar Es Salaam’!


Ndio, sifa ya kwanza ya kuwa ‘ Mzee wa Dar Es Salaam’ ni lazima uwe na zaidi ya miaka 50, uwe mkazi wa Dar Es Salaam kwa miaka isiyopungua 20 mfululizo! Hilo halijaandikwa popote lakini ‘ Wazee’ wenyewe wa jiji wanauzingatia utaratibu huo.


Siku za karibuni kuna “Kijana wa Dar es Salaam” kaninong’oneza kuwa wako mbioni kuwashawishi wazee wa jiji waongeze sifa za kuwa mzee wa Darisalama. Kwamba ili uwe Mzee wa Dar Es Salaam ni sharti, ama uwe umezaliwa na kukulia Dar, au umezaliwa nje ya Dar lakini ujana wako wote umeishi Dar. Hivyo basi, unapoteza sifa ya kuwa Mzee wa Dar es Salaam kama umekuja Dar ukubwani! Marekebisho hayo ya taratibu na sifa yakifanyika, huenda hata mie nitakuwa na sifa ya kuwa Mzee wa Dar es Salaam.


Na Wazee wa Dar Es Salaam wana Mwenyekiti wao. Kwa kawaida siku ya ‘ shughuli’ ya wazee, huvalia kanzu, kibagharashea na kizibau. Ndiye huyu ambaye huwa wa kwanza kumpokea ‘ Mkuu wa Kaya’ anapoingia ukumbini kuwahutubia wazee.


Ni kwa namna gani basi Mwenyekiti wa Wazee wa Dar Es Salaam anachaguliwa?

Jibu: Hilo ni swali la kizushi na usithubutu kuliuliza mbele ya ‘ Wazee wa Dar es Salaam’- watakutoa mbio kwa bakora! Lakini lililo dhahiri ni kuwa, Wazee Wa Dar Es Salaam hawajawahi kuwa na Mwenyekiti mwanamke. Hata Bi. Titi Mohammed hakupata kufikiriwa. Heshima ya kumpa barabara kuitwa kwa jina lake ilitosha, na amshukuru Julius, wanasema Wazee ‘ orijino’ wa Dar Es Salaam.

Ndio, Mkuu yeyote wa Kaya katika nchi hii atashauriwa aongee mbele ya Wazee wa Dar Es Salaam kama ana kubwa analotaka liwafike wananchi. Ni mara moja katika miaka ya karibuni nimemsikia Rais wa nchi akilihutubia taifa kupitia Wazee wa Mkoa wa Dodoma.


Inasemekana jambo hilo liliwashtua baadhi ya Wazee wa wa Dar Es Salaam. Na kuna siku nilitembea kwa miguu mitaa ya Kariakoo Kusini; Livingstone, Mahiwa, Swahili na mingineyo. Hatimaye nikafika kwenye kijiwe cha chai na kahawa pale Mtaa wa Lumumba. Nilianzisha mjadala juu ya Wazee wa Dar Es Salaam. Na hapo nikayasikia manung’uniko.


Ndio, baadhi ya Wazee wa Dar Es Salaam wanaamini kuwa Ilala ndio Dar Es Salaam. Na kwamba ni Wazee wa Ilala ndio waliompokea Julius Nyerere alipoingia mjini. Wanahoji; Iweje Wazee wa ‘ mashambani’ Kinondoni na Temeke nao waitwe Wazee Wa Dar Es Salaam? Swali linabaki; Wazee Wa Dar Es Salaam ni akina nani?


Maggid Mjengwa,

Iringa,

0788 111 765
http://mjengwablog.com

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.