MTANGAZAJI

SAKATA LA UGONJWA WA MWAKYEMBE LACHUKUA SURA MPYA

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii, imemruka Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, na kumtaka aeleze alikoipata taarifa aliyoitoa hivi karibuni kuwa ugonjwa wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, haihusiani na kulishwa sumu.

Wizara hiyo imetoa kauli hiyo siku moja baada ya Dk. Mwakyembe kusema kuwa Jeshi la Polisi limetoa taarifa feki kuhusiana na ugonjwa unaomsumbua tangu Oktoba mwaka jana kuwa hautokani na kulishwa sumu.


Dk. Mwakyembe katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi, alieleza kuwa alichokieleza DCI Manumba hakifanani kabisa na picha iliyo kwenye taarifa halisi ya hospitali inayomtibu ya Apollo nchini India na kuongeza kuwa sumu inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa.


Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, alisema suala hilo limezungumzwa na Manumba, hivyo ni bora atafutwe na kueleza ametoa wapi taarifa hiyo na kueleza kuwa wizara hiyo kwa sasa haina la kusema.


Mponda alisema wizara kama wizara haihusiki katika suala hilo na kuongeza kuwa si haki kuzungumzia ugonjwa wa mtu hadharani. “Naomba usininukuu vinginevyo hao ndiyo waliosema ni vema mkawafuata na kuwauliza nadhani mtapata majibu sahihi,” alisema Waziri Mponda.


Kwa upande wake, Manumba alisema taarifa aliyoitoa mwishoni mwa wiki kuhusiana na ugonjwa wa Dk. Mwakyembe ameipata kutoka kwa madaktari waliokuwa wakimtibu. Hata hivyo hakueleza madaktari hao ni wa hapa nchini au wa nchini India.


Alisema kwa kuwa Dk. Mwakyembe anatibiwa kwa gharama za serikali, ni lazima madaktari wanaomtibu wafikishe taarifa hizo serikalini.


Aidha alisema huu si wakati wa kubishana kwenye vyombo vya habari, kwa kuwa suala hilo linahusiana na ushahidi zaidi, hivyo ni vema ukasubiriwa wakati utakapofika. “Faili tayari limekwishafunguliwa na limefikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, hivyo ni bora mkasubiri upelelezi utakapokamilika na haipendezi kuendelea kuliongelea,” alisema Manumba.


Juzi akihojiwa na Shirika la Utangazaji Nchini (TBC) Taifa kuhusiana na suala hilo, DCI Manumba alisema alichokizungumza kimetokana na madaktari, hivyo kama kuna uongo basi waliosema uongo watakuwa ni hao madaktari.


Akizungumzia suala hilo juzi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Dk. Mwakyembe alisema taarifa halisi ya hospitali ya Apollo inatamka kuwa kuna kitu kwenye uboho (bone marrow) kinachochochea hali aliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaika kukijua, kukidhibiti na kukiondoa.


Alisema kuwa anapata taabu kuamini kama DCI Kanumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matibabu yake au walisoma taarifa feki.


Dk. Mwakyembe alikaririwa akisema anachokiona sasa hasa kutokana na kauli hiyo ya jeshi hilo kuanza kuingilia kati na kutoa taarifa kuhusu ugonjwa unaomsumbua wakati bado hajamaliza matibabu ni mpango wa wazi wa mafisadi kuingilia kwenye suala hilo. Ameeleza kukerwa na tamko hilo la polisi hasa katika hali aliyonayo ya ugonjwa na kushangazwa na ufinyu wa uelewa wa jeshi hilo kusisitiza kuwa hajalishwa sumu wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru.


Amesema amelishangaa jeshi hilo kujiingiza kulizungumzia suala ambalo takriban mwaka mzima halijawahi kuwa na dhamira ya dhati kulichunguza na kulituhumu kwa kulifanyia mzaha jambo hilo kwenye vyombo vya habari. Dk. Mwakyembe alianza kuugua Oktoba mwaka jana na baadaye kupelekwa nchini India na kulazwa kwa matibabu kwa takriban miezi miwili. Alirejea nchini Desemba 11 mwaka jana.


Ugonjwa wake umekuwa ukihusishwa na kulishwa sumu na mara kadhaa Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amenukuliwa akisema ugonjwa huo umetokana na kulishwa sumu na kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi lina ushahidi.


CHANZO: jamiiforums

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.