MTANGAZAJI

TANZANIA INA VYOTE KASORO WATANZANIA

Ndugu zangu,
Jana nilipokea barua kutoka kwa Mtanzania anayeishi Ujerumani. Barua hii imenigusa sana. Imechapwa kwa ujumla kwenye http://mjengwa.blogspot.com . Nitaweka hapa mwanzo tu wa barua husika, kisha nitayasema yangu.
Namnukuu;

“Salaam!
Kaka yangu Mjengwa,

Tangu kuelewa kwangu ubovu huu wa serikali ya Tanzania nimekuwa nikilia kila siku ingawa mtu mzima machozi ni ngumu kutoka. Najipa moyo haya matatizo yataisha siku moja lakini naona sasa nakata tamaa. Hakuna uafadhali na kila siku zikienda ndio kwanza ufisadi unaimarika na mafisadi wanazaliwa pia.

Najiuliza kuna mwisho wa haya? au natakiwa nifanyaje niache kulia? Niko Germany lakini huwa naona aibu nikiulizwa unatoka wapi? “ Mwisho wa nukuu.
Naamini, kuwa nchi yetu ni tajiri sana, lakini watu wake ndio masikini sana. Ni wachache tu ndio wenye kunufaika na utajiri wa nchi yetu. Na jambo hilo hatupaswi tukaliacha liendelee. Angalia picha hizo; wakati Waziri wetu wa Nishati na Madini anaweza kuwa na muda wa kucheza densi kuna watoto wetu kule Songo Songo ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha huku eneo wanaloishi kuna wawekezaji wenye kuvuna gesi yetu na kujitengenezea faida kubwa, tena kwa kukwepa kulipa kodi.
Na mkataba wao wa kuvuna gesi?
Ni miaka 25! Robo karne nzima. Hao Watanzania wenzetu walioshiriki kuingia mikataba hii ya kifisadi huenda hawatakuwepo duniani baada ya robo karne ya wawekezaji kuchota na kukwangua gesi yetu asilia.

Ndugu zangu,
Rasilimali zetu tumeacha zisimamiwe na baadhi ya Watanzania wenzetu wenye hulka za mbweha.
Ni watu wabinafsi na wasio na huruma kwa Watanzania wenzao.

Ndio maana tunasikia kila kukicha kashfa zinazofuatana; Rada, Richmond, IPTL, EPA, Meremeta na nyinginezo nyingi. Ni kashfa zinazowafanya wachache wameremete huku wengi wakifubaa kwenye lindi la umasikini.

Ndio, msingi wake ni ubaguzi wa kisiasa unaotokana na ubinafsi na tamaa ya mali kwa baadhi ya tuliowapa dhamana za kufanya maamuzi makubwa kwa niaba yetu. Ni hali ya baadhi ya tuliowapa dhamana za uongozi kuishiwa chembe chembe za uzalendo; mapenzi kwa nchi yao.Ni watu wenye kulinda maslahi yao na ya wanaowazunguka. Wako tayari hata kutumia mbinu za Umafia kutimiza malengo yao.
Watanzania wengi sasa wanaopoteza moyo wa uzalendo kwa nchi yao. Kuna hata wenye kufikia kutamka; "Nchi hii ina wenyewe". Kuna anayetamka hilo kwa lengo la kumtishia mwenzake au kulazimisha kitu fulani kifanyike. Lakini, kuna wenye kutamka hivyo kuashiria kukata tamaa. Kuwa hata wafanye nini, hakuna anayewasikiliza ama kuwajali. Hizi si dalili njema kwa taifa.

Kuna wanaoiba mali ya umma mchana wa jua kali. Hakuna anayewagusa. Ukiuliza utajibiwa; “Ah! Nchi ina wenyewe!”. Kwamba kuna baadhi yetu hawajisikii kuguswa na nchi hii, hawajisikii kuwa na nguvu ya kupiga vita maovu yanayotusumbua. Baadhi yetu wameanza kupungukiwa na mapenzi na nchi yao. Ni hatari.


Tuna lazima ya kuwa na ujasiri wa kupigania maslahi ya nchi yetu. Ni heri kufa kwa kupigwa risasi kuliko fedheha ya kufa kwa kuumwa na mbu wa Malaria katika nchi ambayo ina rasilimali za kutuwezesha kujenga uwezo wa kuangamiza malaria. Lakini, tunakubali wachache miongoni mwetu wahujumu rasilimali zetu.


Juni 16, 2004 nilipata kuandika hili kwenye gazeti la Majira; kuwa Tanzania ina vyote, kasoro Watanzania. Niliandika; kuwa Tanzania ni nchi nzuri sana. Ni nchi ya kujivunia. Kwamba Tanzania ni nchi kubwa sana kwa eneo. Ni nchi yenye rasilimali nyingi; ardhi yenye rutuba, mito, maziwa, milima, mabonde, bahari na vivutio vingi vya asili. Hata hivyo, Tanzania ni moja ya nchi masikini sana duniani. Kwa nini?


Ndio, kikubwa kinachokosekana Tanzania ni Watanzania. Tanzania tunayoijenga sasa ni mkusanyiko tu wa watu wa makundi mbali mbali wenye kwenda kwa staili ya 'kila mtu na lwake'. idadi ya Watanzania wenye uzalendo na mapenzi kwa nchi yao inazidi kupungua. Ubinafsi umekithiri, na ubinafsi mbaya zaidi ni ule wenye kufanywa na viongozi. Na hilo ni Neno la Leo.


Maggid,

Stockholm, Julai 16, 2011
0736 966032
http://mjengwa.blogspot.com

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.