MTANGAZAJI

JK AFANYA UTEUZI WA NAIBU MAKATIBU WAKUU NA MKURUGENZI WA TBC

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete amefanya uteuzi wa Katibu Mkuu mmoja wa Wizara, Naibu
Makatibu Wakuu 10 wa Wizara mbalimbali na Mkurugenzi wa TBC.

   Aidha, Rais Kikwete amemhamisha Naibu Katibu Mkuu mmoja kutoka
Wizara moja kwenda nyingine.

   Taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar es Salaam, leo, Jumatano, Aprili
27, 2011, na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi Bwana George Yambesi inasema
kuwa uteuzi huo wa maofisa hao waandamizi wa Serikali unaanzia
Alhamisi iliyopita, Aprili 21, mwaka huu, 2011, na wataapishwa
Jumamosi wiki hii, Aprili 30, saa sita mchana.

   Taarifa hiyo inasema kuwa katika uteuzi huo, Rais Kikwete amemteua
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Bwana Job D. Masima kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

   Aidha, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
amemhamisha Injinia Mbogo Futakamba aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara
ya Maji kwenda Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

   Taarifa hiyo inasema kuwa Naibu Makatibu Wakuu walioteuliwa na
Mheshimiwa Rais ni kama ifuatavyo:
       * Bwana Aphayo Kidata ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ikulu.
Kabla ya uteuzi wake, Bwana Kidata alikuwa Mkurugenzi wa Sera na
Mipango katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
       * Bwana Hab Mkwizu ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu
Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kabla ya uteuzi wake, Bwana Mkwizu
alikuwa Karani wa Baraza la Mawaziri.
       * Bwana Charles Amos Pallangyo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Kabla ya uteuzi wake, Bwana Pallangyo
alikuwa Mkurugenzi wa Uratibu – Ofisi ya Waziri Mkuu.
       * Bibi Mwamini Juma Malemi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu
katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kabla ya hapo alikuwa
Msaidizi wa Makamu wa Rais katika masuala ya Maendeleo ya Jamii na
Uratibu wa Malalamiko ya Jamii na Uratibu wa Malalamiko ya Wananchi.
       * Injinia Mussa Ibrahim Iyombe ameteuliwa kuwa Naibu Katibu
Mkuu katika Wizara ya Ulinzi na JKT. Kabla ya uteuzi huo alikuwa
Mkurugenzi wa Miundombinu ya Usafiri katika Wizara ya Ujenzi.
       * Injinia Dkt. John Stanslaus Ndunguru ameteuliwa kuwa Naibu
Katibu Mkuu katika Wizara ya Ujenzi. Kabla ya hapo, alikuwa Mkurugenzi
wa Huduma na Ufundi katika wizara hiyo hiyo ya Ujenzi.
       * Bwana John Thomas James Mngodo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu
Mkuu katika Wizara ya Uchukuzi. Kabla ya uteuzi wake alikuwa
Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula.
       * Bibi Anna T. Maembe ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Kabla ya uteuzi wake,
Bibi Maembe alikuwa Mkurugenzi wa Mazingira na Habari wa NEMC.
       * Bibi Sihaba Nkinga ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Kabla ya hapo alikuwa
Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Uchukuzi.
       * Injinia Bashir J. Mrindoko ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu
katika Wizara ya Maji. Kabla ya uteuzi wake, Bwana Mrindoko alikuwa
Kamishna wa Nishati na Mafuta ya Petroli.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bwana Clement Senzota Mwete Mshana kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.