MTANGAZAJI

RAIS KIKWETE KUSHIRIKI MKUTANO WA EITI PARIS,UFARANSA

Rais Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kutoa mada juu ya umuhimu wa shughuli za uziduaji na uwazi katika mapato ya madini katika mkutano wa Kimataifa wa Tasnia ya Uziduaji, (Global Extractive Industries Transparency Initiative -EITI), ambayo ina malengo ya kuongeza uwazi na uwajibikaji katika mapato yatokanayo na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia. 

Mkutano huo wa siku mbili unaanza kesho, Jumanne, Machi 2, 2011 jijini Paris, Ufaransa, na Rais Kikwete anaondoka nchini leo asubuhi kwenda kuhudhuria mkutano huo.


Tanzania iliomba na kupewa uanachama wa muda wa EITI tangu mwaka 2009. Tanzania itaweza kupata uanachama kamili baada ya kuwa imekamilisha na kutimiza vigezo vya kuwa mwanachama kamili na kuweka misingi ya utoaji taarifa hizo muhimu kwa umma juu ya malipo ya kodi kutoka makampuni mbalimbali yaliyopo nchini.

Lengo kuu la kujiunga na EITI ni kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia kwa kutangaza hadharani malipo yanayotokana na rasilimali zake kwa manufaa ya wananchi wake
.

Utaratibu huu utaweka uwazi na kuondoa usiri ambao unaweza kuwa mwanya wa kuficha mapato halisi ya makampuni husika.

Baada ya kumaliza mkutano huo wa Paris, Ufaransa, Rais Kikwete atasafiri kwenda moja kwa moja Nouakchott, Mauritania kwa ajili ya kikao cha marais wa Afrika wanaotafuta suluhisho la tatizo la kisiasa katika Ivory Coast.

Katika Mauritania, Rais Kikwete atajiunga na marais wa Mauritania, Afrika Kusini, Burkina Faso, Chad, Nigeria na Equatorial Guinea pamoja na wawakilishi wa Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Balozi Jean Ping na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN).

Katika kikao hicho, viongozi hao watafikia uamuzi wa AU kuhusu mzozo huo na kupendekeza namna gani ya kuutatua mzozo huo uliolipuka kufuatia raundi ya pili ya upigaji kura katika Uchaguzi Mkuu wa Ivory Coast Novemba 28, mwaka jana, 2010

Matokeo yake, nchi hiyo imegawanyika katika sehemu mbili, moja ikimuunga mkono aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, Mheshimiwa Alassane Quattara na nyingine ikimuunga mkono Rais aliyekuwa anatetea kiti chake katika uchaguzi huo, Mheshimiwa Laurent Gbagbo.

Kila mmoja kati ya wanasiasa hao amejitangaza kuwa Rais na kila mmoja ameunda na kutangaza Serikali katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.


Wiki iliyopita, viongozi hao wa Afrika walikutana mjini Nouakchott na baadaye wakaenda Abidjan, Ivory Coast ambako walikutana na viongozi hao wawili nchini humo katika jaribio la kutafuta suluhisho la mzozo huo.


Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM

01 Machi, 2011

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.