MWONGOZO WA KANISA LA WAADVENTISTA KUFANYIWA MAREKEBISHO KABLA YA MWAKA 2030.
Wajumbe wa Baraza la mwaka la Kanisa la Waadventista wa Sabato wamepitisha hoja muhimu ya kuanza mapitio ya kina ya Mwongozo wa Kanisa hilo ambao ni Kanuni Kuu zinazoongoza utendaji wa kanisa duniani.
Hoja hiyo iliwasilishwa na Gerson Santos, Katibu Msaidizi wa Konferensi Kuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato ulimwenguni , ambaye alieleza kuwa mchakato huo unalenga kuandaa toleo jipya la mwongozo huo litakalowasilishwa kwa kupigiwa kura katika Mkutano Mkuu wa Kanisa hilo dunia mwaka 2030 utaofanyika Indianapolis, Indiana, Marekani.ukiwaleta pamoja wajumbe wa kutoka katika nchi mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa Santos, kazi kubwa inatarajiwa kufanyika katika kipindi cha miaka miwili ijayo ili rasimu ya kwanza iwe tayari kufikishwa kwenye Baraza la Mwaka 2028, na baadaye kurejeshwa tena mwaka 2029 kwa mapitio ya mwisho kabla ya kuingizwa kwenye ajenda ya Mkutano Mkuu wa mwaka 2030.
Kamati ya Mwongozo wa Kanisa ilishakutana Septemba 15 na kupendekeza mapitio ya kina, ikisisitiza lugha rahisi ya maudhui, kupunguza marudio, na kubainisha kwa uwazi tofauti kati ya kanuni zinazotumika kwa kanisa la ulimwengu mzima na taratibu zinazoweza kutofautiana kulingana na eneo. Mapendekezo hayo yanatarajiwa kujumuisha maoni ya wachungaji, viongozi wa makanisa ya eneo, na wadau wengine duniani kote.
Baadhi ya waliokuwa viongozi na waliopo sasa waliokuwapo kwenye kikao walitoa maoni mbalimbali. Baadhi walipongeza ujasiri wa kuanzisha mchakato huo, huku wengine wakitaka ufafanuzi zaidi kuhusu muda na upeo wa marekebisho.
Kiongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni Erton Köhler, alisisitiza kuwa mapitio hayo hayatalenga kubadili imani za msingi za kanisa, bali kurahisisha mwongozo ili uwe wazi, unaoeleweka, na wa vitendo kwa makanisa.
Hoja hiyo hatimaye ilipitishwa kwa kura 167 dhidi ya 32.
Mwaka 2008 mapendekezo ya kufanya marekebisho ya kina kwa Mwongozo wa kanisa hilo yalitolewa, ambapo mwaka 2019 pendekezo jingine la marekebisho lilitolewa lakini janga la Uviko-19 lilichelewesha mchakato huo na mwaka 2022 hadi 2025 toleo la 20 na 21 la Mwongozo wa Kanisa lilifanyiwa maboresho ya kawaida ikiwemo kusasisha vipengele 29 vilivyokuwa vinajirudia.

.png)
Post a Comment