VIONGOZI WAPYA KANISA LA WAADVENTISTA WA SABATO ECD
Kamati ya Utendaji ya Konferensi Kuu (GC) ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni ilipiga kura mnamo Novemba 2, 2026, kumuidhinisha Dkt. Moses Ndimukika Maka kuwa Mwenyekiti mpya wa Kanisa la Waadventista wa Sabato katika Divisheni ya Afrika ya Mashariki na Kati (ECD), na Dkt. Tom Ogal kuwa Katibu Mtendaji.
Upigaji kura huo ulifanyika wakati wa mkutano wa Kamati ya Utendaji ya GC ulioendeshwa kwa njia ya mtandao wa intaneti ukiwakutanisha wajumbe wake walioko katika nchi mbalimbali duniani, kufuatia uteuzi wa viongozi hao wawili na Kamati Utendaji ya ECD iliyofanya kikao chake Oktoba 29 mwaka huu.
Maka na Ogal, ambao walikuwa wakihudumu kwa nafasi ya Katibu Mtendaji wa ECD na Naibu Katibu wa ECD mtawalia tangu mwaka 2025 na wataanza kutekeleza majukumu yao mapya mara moja. Mwenyekiti wa zamani wa ECD, Blasious Ruguri, ataendelea kuhudumu katika nafasi ya mshauri hadi atakapostaafu Disemba 31 mwaka huu.
Kuchaguliwa kwa viongozi hao wawili kulikuwa kukisubiriwa kwa hamu na waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato katika Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati inayoelezwa kuwa na idadi kubwa ya waumini waadventista, kufuatia kutangazwa kustaafu kwa Ruguri ambaye aliongoza Divisheni hiyo kwa miaka 16.
Takwimu za hivi karibuni za Divisheni ya Afrika ya Mashariki na Kati (ECD) hadi Juni 30, 2025 zinaonyesha kuwa ECD inawaumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato 5,857,831, Makanisa 21,754 katika idadi ya watu wapatao 523,995,000 walioko katika eneo hilo linalojumuisha nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Uganda, na Tanzania.

.png)
Post a Comment