MTANGAZAJI

KIM SUNHWAN MWENYEKITI MPYA WA DIVISHENI YA KASKAZINI YA ASIA- PASIFIKI


Kim SunHwan amechaguliwa kuwa mwenyekiti  mpya wa Divisheni ya Kaskazini ya Asia-Pasifiki ya Kanisa la Waadventista wa Sabato (NSD) katika kikao cha Baraza kuu la mwaka la Kanisa hilo  Ulimwenguni  Oktoba 13 mwaka huu.
 
Kamati Kuu ya Utendaji ya NSD, ambayo hufanya kazi ya  kamati ya uteuzi kati ya vikao vya Baraza Kuu, ilimpendekeza Kim kwa Kamati ya Utendaji ya Baraza Kuu. Baada ya majadiliano yaliyosisitiza uwajibikaji, uwazi na haki, wajumbe wa mataifa mbalimbali katika kanisa la Waadventista  waliidhinisha rasmi uteuzi wake.
 
Kim anachukua nafasi ya Kang SoonGi, ambaye kujiuzulu kwake kulikubaliwa  Oktoba 9, mwaka huu. Divisheni ya NSD inasimamia kazi ya kanisa hilo katika nchi na maeneo tisa, katika eneo lenye watu takribani milioni 700 wakiwemo zaidi ya Waadventista 365,000.
 
Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Kim alisema anajisikia mnyenyekevu na anaona uzito wa jukumu analolichukua, hasa wakati huu wa changamoto katika divisheni hiyo. Hata hivyo, alisisitiza kuwa anakubali wito huo kwa imani, akitegemea ahadi ya Warumi 11:29 kwamba karama na mwito wa Mungu havibatiliki. Kim amewaomba waumini na viongozi waendelee kumkumbuka katika maombi.
 
Mwenyekiti wa Baraza Kuu na Kiongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Duniani, Erton Köhler, amemkaribisha Kim akimtaja kuwa kiongozi mwenye mizani na mwenye mtazamo wa utume, sifa muhimu kwa kanisa katika kipindi hiki.
 
Kim SunHwan analeta uzoefu wa zaidi ya miaka 30 katika uongozi wa kanisa. Kabla ya kuchaguliwa, alikuwa Mwenyekiti wa Kanisa hilo wa Fildi ya Misri tangu Agosti 2025. Pia amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya NSD, ikiwemo mkurugenzi wa Utume wa Kiadventista, Idara ya masuala ya umma na uhuru wa dini (PARL), huduma ya Walei Waadventista na wamiliki wa viwanda (ASI), na katibu msaidizi wa divisheni.
 

Kim amewahi kuwa mchungaji kiongozi wa kanisa la Kiingereza la Ilsan katika Konferensi ya Korea ya Kati‑Magharibi. Pia amewahi kuwa Katibu Mtendaji katika shule ya Waadventista inayofundisha lugha nchini Korea, kabla ya kuwa mkurugenzi wa kituo chake cha lugha kilichopo nchini Ufilipino.

Mchungaji huyo alihusika katika kesi ya kihistoria ya Mahakama Kuu ya Korea Kusini mwaka 2019 kuhusu utunzaji wa Sabato, ambayo ilileta mafanikio makubwa katika kulinda uhuru wa watu wanaotunza siku ya Sabato nchini humo.
 
Kim ana shahada ya theolojia kutoka Chuo Kikuu cha  Sahmyook, shahada ya uzamili kutoka AIIAS nchini Ufilipino, na hivi karibuni amekamilisha shahada ya uzamivu katika utume na injili. Ameoana na  Park SookJa, wana watoto wawili  na wajukuu wawili.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.