MTANGAZAJI

UONGOZI WA KANISA LA WAADVENTISTA WATOA SHUKRANI KWA WAUMINI

 

Uongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni umetoa shukrani kwa waumini wake kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa kuendelea kuonyesha kujitoa kwao katika kueneza injili kupitia ongezeko kubwa la msaada wa utume kwa njia ya matoleo ya sadaka ya utume.

Ripoti iliyowasilishwa katika Baraza la Mwaka lililomalizika hivi karibuni nchini Marekani inaonyesha kuwa hadi Agosti 2026, Makao Makuu ya Kanisa la Waadventista (GC) yamepokea zaidi ya dola za kimarekani milioni 72.8 za sadaka za utume. Kiasi hicho ni ongezeko la karibu asilimia 10 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa Mweka Hazina wa GC, Paul Douglas, mafanikio haya yanatokana na ukarimu wa washiriki wa kanisa wanaotoa kwa moyo ili kuendeleza kazi ya wamishonari, kuimarisha shule, makanisa, na kushiriki injili katika jamii mbalimbali duniani.

Douglas amesema kuwa licha ya changamoto za kiuchumi zinazoendelea duniani, Mungu ameendelea kutoa rasilimali zinazohitajika ili kazi ya utume iendelee.

“Kuna wasiwasi mwingi wa kiuchumi, lakini Mungu ametoa rasilimali tunazohitaji kwa ajili ya misheni Yake,” amesema Douglas.

Naibu Mweka Hazina wa GC, Ray Wahlen, ameeleza kuwa sadaka za utume husaidia maeneo ambayo hayana uwezo wa kifedha kuendesha huduma za kanisa. Fedha hizo hutumika kujenga shule, mabweni, makanisa, kuendeleza programu za uinjilisti, pamoja na kuunga mkono vyuo na huduma za vyombo vya habari vya kanisa hilo..

Wahlen ameongeza kuwa msaada huu wa pamoja unawawezesha wamishonari wanaofanya kazi katika tamaduni mbalimbali kuendelea na huduma, hasa katika maeneo ambayo hayana uwezo wa kujitegemea.

“Tunawashukuru washiriki wa kanisa duniani kote kwa kuendelea kuunga mkono sadaka za utume. Ukarimu wao umewezesha kanisa kupanuka na kuwafikia watu wapya kwa ajili ya ufalme wa Mungu,” amesema Wahlen.

Sadaka za utume hukusanywa kupitia Shule ya Sabato na mipango mingine ya utoaji. Ingawa njia za kukusanya sadaka hutofautiana katika maeneo mbalimbali, lengo linabaki kuwa moja kushirikiana rasilimali ili kuendeleza utume dunia nzima.

Historia inaonyesha kuwa utamaduni huu wa kushirikiana ulianza mapema, ikiwemo mwaka 1890 wakati sadaka za Shule ya Sabato zilitumika kujenga meli ya utume  Pitcairn, iliyowafikisha wamishonari wa kiadventista katika Kisiwa cha Pitcairn na kuanzisha kanisa huko.

Njia za kufikisha injili zimeongezeka, lakini kanuni ya kushirikiana rasilimali bado ni msingi wa kazi ya kanisa hilo. Sadaka za mara kwa mara husaidia kuendeleza shule, makanisa mapya, na kuwasaidia wamishonari wakati wote wa huduma yao.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.