MTANGAZAJI

WALIMU NCHINI KUAJIRIWA MOJA KWA MOJA

SERIKALI imeamua kuwa kuanzia sasa walimu nchini, kama ilivyo kwa madaktari, wataajiriwa na kupangiwa moja kwa moja vituo vya kazi bila kufanya usaili ama kucheleweshwa na michakato na taratibu nyingine za kirasimu, ili mradi wawe wameshinda mitihani yao.


Ili kutekeleza uamuzi huo wa Serikali, imeamuliwa kuwa walimu watapangiwa vituo vya kazi katika miezi ya mwisho ya mafunzo yao ili kuwawesha kuripoti moja kwa moja kwenye vituo vyao baada ya kumaliza masomo na mafunzo yao.


Uamuzi huo wa Serikali ulifikiwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika wiki iliyopita, Alhamisi, Februari 3, 2011, mjini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.


Baraza limefikia uamuzi huo kwa kutilia maanani uhaba wa walimu, kama walivyo madaktari nchini na, kwa nia ya kupanua na kuboresha kiwango cha huduma elimu.

(Phillemon L. Luhanjo)

KATIBU WA BARAZA LA MAWAZIRI

07 FEBRUARI, 2011

1 comment

Filipo Lubua said...

Bwana Mtangazaji,

Hii ni danganya toto tu ya serikali baada ya kuona shule nyingi hazina walimu na wakati huohuo wao wamechelewa kuwaajiri walimu wengi. Ukweli ni kwamba hata miaka ya nyuma walimu wamekuwa wakiajiriwa bila usaili wowote maana hata mimi mwenyewe nilipewa kazi hiyo pasipo hata kuiomba.

Wakati tunafikia mwisho wa kukamilisha shahada zetu, mwaka 2009, serikali ilitoa tangazo kuwa wanaotaka waombe kazi ya ualimu. Mimi sikuomba lakini walinipangia Mtwara (japokuwa sikwenda). Sasa hilo swala wanalosema eti watawaajiri walimu bila usaili, ni la kutapatapa tu. Waboreshe masilahi ya waalimu, hasa walio vijijini waone kama watu hawatakwenda kufanya kazi hiyo kwa moyo mmoja.

Mtazamo News . Powered by Blogger.