VISIT ZANZIBAR SASA KWENYE MABASI YA ABIRIA UINGEREZA
Zanzibar inatarajia kutangaza vivutio vya utalii wake kwa kutumia mabasi ya abiria ya Uingereza ikiwa ni mkakati wake wa kutangaza sekta hiyo nchi za nje hasa barani Ulaya.
Picha zilizowekwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ), Haji Haji katika mtandao wa kijamii wa Linkedin zinaonesha baadhi ya mabasi ya abiria yakiwa kwenye karakana jijini London , Uingereza na yamechorwa vivutio vya utalii adimu wa visiwa hivyo na kuandikwa "Visit Zanzibar" kila upande wa mabasi hayo.
Jiji la London (Uingereza) lenye takribani watu milioni 9 kulingana na makadirio ya hivi karibuni huku tovuti nyingine za takwimu zinaonyesha makadirio ya mwaka 2026 kuwa karibu watu karibu milioni 10. Huku jiji hilo likiwa ni miongoni mwa miji inayotembelewa zaidi duniani, ikiwa na takribani milioni 21.7 milioni ya watalii wa kimataifa kwa mwaka ambao miongoni mwao kwa asilimia kubwa hutumia mabasi ya umma.
Hivi karibuni serikali ya Zanzibar kupitia mtandao wa Instagram katika ukurasa wake wa Ikulu ilieleza kuwa na ongezeko kubwa la utalii visiwani humo,ambapo watalii wa kimataifa kwa mwaka 2020 walikuwa ni 260,644 na mwaka 2025 walikuwa ni 910,682, ambalo ni ongezeko la watalii 650,038.
Twakwimu hizo zinaonesha kuwa mwaka 2021 kulikuwa na watalii 394,185 huku mwaka 2022 ukishuhudia watalii wapatao 548,503 ambapo watalii 638,498 waliingia Zanzibar mwaka 2023. Mwaka 2024 kulikuwa na watalii 736,755.


Post a Comment