MTANGAZAJI

NUSU YA MAREKANI YATISHIWA NA DHORUBA KALI YA BARIDI.

 


Mvua ya barafu imenyesha katika maeneo kadhaa ya jimbo la Texas siku ya Ijumaa, huku dhoruba kubwa ya majira ya baridi ikianza safari ya siku kadhaa ambayo inatarajiwa kuathiri takribani nusu ya wakazi wa Marekani. Watabiri wa hali ya hewa wameonya kuwa dhoruba hiyo italeta theluji, mvua ya barafu, baridi kali na kukatika kwa umeme kwa kiwango kikubwa, huku uharibifu hasa katika maeneo yatakayopigwa na barafu ukielezwa kuwa unaweza kulinganishwa na ule wa kimbunga.

Shule,vyuo na ofisi za umma katika majimbo kadhaa ya Kati ya Magharibi na kusini mwa Marekani zimesitisha masomo kuanzia ijumaa hadi jumatatu, mashirika ya ndege yameahirisha maelfu ya safari za mwishoni mwa juma, makanisa yamehamishia ibada mtandaoni, na matukio mengine yanayohusisha mikusanyiko ya watu yemefutwa ama kuahirishwa.

Kwa mujibu wa mamlaka za hali ya hewa nchini Marekani, watu wasiopungua milioni 182 wako chini ya tahadhari au onyo la theluji na barafu, huku zaidi ya milioni 210 wakiwa chini ya tahadhari za baridi kali na katika maeneo mengi tahadhari hizo zinaingiliana. Kampuni za umeme zimejiandaa kukabiliana na kukatika kwa huduma, kwani miti na nyaya za umeme zinazofunikwa na barafu zinaweza kuanguka hata baada ya dhoruba kupita.

“Mfumo huu wa hali ya hewa ni mkubwa,” alisema Maricela Resendiz alipokuwa akinunua chakula katika duka moja mjini Dallas ili kujitayarisha yeye, mwanawe wa miaka mitano na mume wake kwa ajili ya mwisho wa juma. Alisema mipango yake ni kubaki nyumbani na kuepuka hatari. Huko Lubbock, Texas, mvua ya barafu ilifanya barabara ziwe za utelezi huku joto likishuka.

Baada ya kusogea kuelekea kusini, dhoruba hiyo inatarajiwa kuelekea Kaskazini Mashariki mwa Marekani, ikimwaga takribani sentimita 30 za theluji kuanzia Washington hadi New York na Boston, kwa mujibu wa Mamlaka ya Huduma ya Kitaifa ya Hali ya Hewa. Upepo mkali wa baridi kutoka Canada umesababisha kufutwa kwa masomo katika shule nyingi za Kati ya Magharibi. Ubaridi unaohisiwa kufikia hadi nyuzi joto hasi 40 za Fahrenheit sawa na hasi 40 za Selsiasi unaweza kusababisha baridi kali kuathiri ngozi ndani ya dakika 10, hali inayofanya iwe hatari kutembea au kusubiri usafiri.

Hata hivyo, licha ya baridi kali, maandamano dhidi ya operesheni kali ya uhamiaji yameendelea kama ilivyopangwa huko Minnesota, ambapo maelfu walikusanyika katikati ya jiji la Minneapolis.

Kitaifa, zaidi ya safari 1,000 za ndege ziliripotiwa kuchelewa au kufutwa siku ya Ijumaa, zaidi ya nusu zikiwa Dallas, kwa mujibu wa tovuti ya FlightAware. Takribani safari 2,300 zilifutwa kwa siku ya Jumamosi.

Huko Oklahoma, wafanyakazi wa idara ya usafirishaji walirekebisha barabara kwa mchanganyiko wa chumvi, Polisi wa barabarani walifuta mapumziko ya askari, na vikosi vya Ulinzi wa Taifa viliamshwa kusaidia madereva waliokwama.

Serikali ya shirikisho imeweka karibu timu 30 za utafutaji na uokoaji katika hali ya tahadhari. Pia, zaidi ya milo milioni saba, blanketi 600,000 na jenereta 300 vimewekwa tayari katika maeneo yatakayopitiwa na dhoruba hiyo, kulingana na Shirika la Usimamizi wa Dharura la Marekani, FEMA.

Rais Donald Trump amesema kupitia mitandao ya kijamii kuwa serikali yake inashirikiana kwa karibu na viongozi wa majimbo na serikali za mitaa, na kwamba FEMA iko tayari kikamilifu kukabiliana na athari za dhoruba hiyo.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.