ZAMBIA YAZINDUA RASMI MFUMO WA KIDIJITALI WA MAOMBI YA PASI ZA KUSAFIRIA.
Serikali ya Zambia imezindua rasmi mfumo wa mtandaoni wa kuomba na kulipia pasi za kusafiria kupitia ZamPortal, hatua inayochukuliwa kuwa ni mafanikio katika safari ya taifa hilo ya mageuzi ya kidijitali. Mfumo huu mpya unawawezesha wananchi kuomba pasi za kusafiria na nyaraka nyingine za kusafiria kutoka mahali popote na wakati wowote, huku ukitoa huduma salama, ya haraka na inayomlenga mwananchi.
Akitoa tangazo hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Ndani wa Zambia, Jack Mwiimbu, alieleza kuwa mpango huo unaendana na ajenda pana ya serikali ya mageuzi ya kidijitali, inayoongozwa na Taasisi ya Smart Zambia kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango ya Kitaifa.
Mfumo wa kidijitali wa pasi za kusafiria umebuniwa ili kukabiliana na changamoto zilizokuwepo katika mfumo wa jadi wa maombi ya ana kwa ana, ikiwemo foleni ndefu, gharama kubwa za usafiri na kupotea kwa muda wa uzalishaji, hususani kwa waombaji wanaoishi maeneo ya mbali ukilenga kuongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wote.
Kwa sasa, jukwaa la mtandaoni linawezesha maombi ya pasi za kusafiria za Zambia, pasipoti za kidiplomasia, nyaraka za kusafiria kwa wakimbizi, hati maalum ya kusafiria kwa kuvuka mipaka kati ya nchi wanachama wa COMESA, na nyaraka nyingine za utambulisho wa kusafiria. Muda wa uchakataji umewekwa kuwa siku 14 kwa Lusaka, Ndola na Livingstone, na siku 21 kwa miji mikuu mingine ya mikoa. Katika kipindi cha mpito, maombi ya mfumo wa kawaida yataendelea sambamba na mfumo wa mtandaoni.
Hatua hii inaakisi dhamira ya Zambia katika kutumia teknolojia kurahisisha huduma za umma, kuongeza upatikanaji wa huduma, na kuboresha uzoefu wa wananchi kote nchini humo.
Baadhi ya nchi za Afrika ambazo tayari zimeanzisha au zinatumia mfumo wa mtandaoni wa kuomba na kulipia pasi za kusafiria ni pamoja na Kenya ,Tanzania, Nigeria, Ghana, Rwanda,Uganda, Afrika Kusini, Botswana na Morocco.

.png)
Post a Comment