MTANGAZAJI

SAFARI ZA ULAYA - MAREKANI KUBADILIKA

 


Serikali ya Marekani imetangaza mabadiliko mapya ya taratibu za uingiaji nchini humo, hatua inayolenga kuimarisha ukaguzi wa usalama kwa wasafiri kutoka Ulaya na mataifa mengine yanayotumia Visa Waiver Program (VWP)

VWP ilianza kutumika mwaka 1986 nchini Marekani.Hapo mwanzo iliitwa Visa Waiver Pilot Program, ikiwa ni mpango wa majaribio uliowezesha raia wa nchi chache kusafiri Marekani bila visa kwa ziara fupi. Baadaye, kutokana na mafanikio yake, Marekani ilipitisha sheria ya kuufanya mpango huu kuwa wa kudumu kupitia mwaka 2000 kwa raia wanaotoka nchi 42 hasa barani Ulaya, kwa safari za utalii na biashara kwa siku 90 nchini Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa za Idara ya Usalama wa Ndani, wasafiri wote watakaotumia mfumo huo sasa watatakiwa kuwasilisha historia ya matumizi ya mitandao ya kijamii ya takribani miaka mitano iliyopita, pamoja na barua pepe na namba za mawasiliano zilizotumika katika kipindi hicho. Lengo kuu, kwa mujibu wa maafisa wa serikali, ni kuboresha uwezo wa uchunguzi kabla ya msafiri kuruhusiwa kupanda ndege kuingia Marekani.

Katika hatua nyingine, kuanzia mwishoni mwa mwaka huu, utaratibu wa kukusanya taarifa za kibaiometriki utafanywa kwa wasafiri wote ikijumuisha kupigwa picha na kuchukuliwa alama za vidole wakati wa kuingia na hata kutoka nchini humo. Hatua hii inatajwa kuwa sehemu ya maboresho ya mfumo wa Ulinzi wa Mipaka.

Hata hivyo, mashirika ya utalii yameeleza wasiwasi kwamba masharti haya mapya huenda yakapunguza idadi ya watalii kutoka Ulaya, hasa wale wanaoona utoaji wa taarifa za mitandao ya kijamii kama uvamizi wa faragha.

Licha ya mabadiliko hayo, raia wa Ulaya wanaotumia Visa Waiver  wataendelea kuruhusiwa kuingia Marekani bila visa kwa ziara za hadi siku 90, mradi watimize masharti mapya ya uchunguzi wa usalama.

Kwa sasa, pendekezo kuhusu upokeaji wa historia ya mitandao ya kijamii linapitia maoni ya umma kabla ya kuanza kutekelezwa rasmi.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.