AWR AFRIKA KUFADHILI UANZISHWAJI WA KITUO CHA RADIO CHUO KIKUU CHA ARUSHA
Radio ya Waadventista Ulimwenguni (AWR) kanda ya Afrika imeingia makubaliano na Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania katika Kanisa la Waadventista wa Sabato (NTUC) kufadhili uanzishwaji wa kituo kipya cha Radio cha AWR katika Chuo Kikuu cha Arusha (UoA), Tanzania.
Makubaliano hayo yamefanyika wakati wa mahafali ya 19 ya Chuo Kikuu cha Arusha kinachomilikiwa na Kanisa hilo yaliyofanyika Novemba 28-30 chuoni hapo, ambapo AWR iliwakilishwa na Mkurugenzi wake katika kanda ya Afrika, Immanuel Ogwal huku NTUC ikiwakilishwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Gideon Msambwa.
Ogwal amesisitiza kuwa ili kuwafikiwa watu wengi zaidi katika ujumbe wa matumaini na kubadilisha maisha, ni muhimu kuanzisha kituo cha redio kinachozalisha maudhui bora ya kiroho yatakayoifikia jamii.
Kituo hicho kitapewa jukumu la kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosomea kozi za mawasiliano na vyombo vya habari chuoni hapo, ili kuwatayarisha katika taaluma na kuongeza ufanisi wa huduma ya utume.
Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania linamiliki Shirika la Vyombo vya Habari vya kanisa hilo nchini humo (TAMC) lenye makao yake makuu jijini Dar es salaam, likisimamia kituo cha Televisheni cha Hope Channel Tanzania na kituo cha Radio cha AWR chenye studio zake kadhaa ikiwemo Morogoro, Mtwara na kituo cha Radio cha Rock FM cha jijini Mbeya.

.png)
Post a Comment