MAREKANI YARAHISISHA VISA KWA WAGENI WA KOMBE LA DUNIA
Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump umetangaza mpango mpya kwa wageni wanaosafiri kwenda Marekani kwa Kombe la Dunia la mchezo wa soka mwakani, ambao utawezesha kupata mahojiano ya visa ya Marekani kwa haraka zaidi.
Mpango huo, unaoitwa “FIFA Pass”, utawawezesha wale walionunua tiketi za Kombe la Dunia kupitia FIFA kupata miadi ya visa kwa haraka, huku utawala ukijaribu kusawazisha sera kali za uhamiaji za Rais Trump na ongezeko la wasafiri wa kimataifa wanaoingia Marekani kushuhudia mashindano ya soka. Neno “pass” lililotumika kwenye jina linamaanisha “mfumo wa kupanga miadi kwa kipaumbele.”
Rais wa FIFA, Gianni Infantino, aliyekuwa na Trump Jumatatu, alisema: “Ikiwa una tiketi ya Kombe la Dunia, unaweza kupata miadi ya kipaumbele kupata visa yako.” Akimzungumzia Rais wa Marekani, aliongeza: “Ulisema mara ya kwanza tulipokutana, Mheshimiwa Rais, Amerika inakaribisha dunia.”
Trump alisema Jumatatu kuwa anahimiza sana wasafiri wanaopnga kwenda Marekani kwenye mashindano ya Kombe la Dunia kuchukua visa zao mara moja.
Marekani imetuma maafisa zaidi ya 400 wa balozi zake duniani kote kushughulikia mahitaji ya visa, na kuwa katika takriban asilimia 80 ya dunia, wasafiri wanaweza kupata miadi ya visa ndani ya siku 60. Kwa mfumo mpya, wale walionunua tiketi kupitia FIFA wataruhusiwa kupitia “mlango wa FIFA” ambao utasaidia kupanga maombi yao ya visa na mahojiano kwa kipaumbele.
Wakati wa Kombe la Dunia mwakani, michezo 104 itachezwa Canada, Mexico na Marekani. Trump ameweka mafanikio ya Kombe la Dunia kuwa kipaumbele chake, na Infantino amekuwa akitembelea Ikulu mara kwa mara huku FIFA ikiandaa droo ya Kombe la Dunia Disemba katika taasisi ya sanaa ya Kennedy Center, inayosimamiwa na wafuasi wa Trump.
Trump pia alionyesha uwezekano wa kuhamisha michezo ya Kombe la Dunia kutoka moja ya miji yenyeji iwapo ataona haiko salama, kutokana na uteuzi wa mtoa maoni wa kijamii Katie Wilson kutoka Seattle, ambaye ameeleza mpango wa “kulinda mji dhidi ya sera za Trump” na kuhifadhi hadhi ya mji salama kwa wahamiaji. Seattle ni moja ya miji 11 ya mwenyeji wa mashindano hayo nchini Marekani mwakani.
“Ikiwa tutadhani kuna ishara ya matatizo yoyote, ningeomba Gianni kuhamisha hiyo michezo kwenda mji mwingine,” Trump alisema kuhusu Seattle. Rais wa FIFA aliepuka kujibu moja kwa moja kuhusu uhamisho wa miji, akibainisha kuwa: “Nadhani usalama ndio kipaumbele cha kwanza kwa Kombe la Dunia kufanikiwa,” na kuongeza: “Tunaweza kuona leo kuwa watu wana imani na Marekani,” akitaja idadi ya tiketi ambazo tayari zimeshauzwa.

.png)
Post a Comment