MTANGAZAJI

META YATOA ANGALIZO KWA WATOTO AUSTRALIA

 


Kampuni ya teknolojia Meta imeanza kuwatumia maelfu ya vijana nchini Australia ujumbe wa onyo kwa majuma mawili kuanzia Novemba 20 mwaka huu, ikiwataka kupakua kumbukumbu zao na kufuta akaunti zao za Facebook, Instagram na Threads kabla ya marufuku ya kwanza duniani ya mitandao ya kijamii kwa watoto chini ya miaka 16 kuanza kutekelezwa.

Serikali ya Australia ilitangaza majuma mawili yaliyopita kuwa majukwaa ya Meta pamoja na Snapchat, TikTok, X na YouTube lazima yachukue hatua kuhakikisha watoto walio chini ya miaka 16 hawafungui akaunti kuanzia Disemba 10.

Meta imekuwa kampuni ya kwanza kuelezea jinsi itakavyotekeleza sheria hiyo, ambapo Novemba 20 ilianza kuwasiliana na maelfu ya watumiaji vijana kupitia SMS na barua pepe, ikionya kuwa watakaoshukiwa kuwa chini ya umri huo watazuiwa kuingia kuanzia Disemba 4,2025

Meta imesema tangazo hilo litawapa vijana nafasi ya kuhifadhi kumbukumbu zao na taarifa zao muhimu, na pia kusasisha mawasiliano yao ili waweze kurejeshewa akaunti watakapofikisha miaka 16. Kampuni hiyo inakadiria kuwa kuna vijana takriban 350,000 wenye umri wa miaka 13 hadi 15 kwenye Instagram, na 150,000 kwenye Facebook nchini Australia.

Kwa wale walio na miaka 16 au zaidi lakini wakapokea onyo kimakosa, watahitajika kuthibitisha umri wao kupitia kampuni ya Yoti kwa kutumia kitambulisho cha serikali au video inayonesha sura ya mhusika.

Mtaalamu wa masuala ya Akili Unde (AI) kutoka Chuo Kikuu cha Sydney, Profesa Terry Flew, amesema teknolojia ya utambuzi wa sura ina kiwango cha makosa kisichopungua asilimia 5, na kwamba ukosefu wa kitambulisho cha kitaifa unalazimisha kutumia njia zisizo kamilifu.

Serikali imesema kuwa kutaka kila mtumiaji athibitishe umri wake kwa lazima kungekuwa kuzidisha viwango vya udhibiti. Hata hivyo, majukwaa yanaweza kutozwa faini ya hadi dola milioni 50 za Australia endapo hayatadhibiti akaunti za watoto wadogo.

Mkuu wa usalama wa Meta duniani, Antigone Davis, amesema angependa majukwaa ya kupakua programu tumizi kama Apple App Store na Google Play yawajibike kukusanya umri wa watumiaji na kuhakikisha wana miaka 16.

Kwa upande wa wazazi, Dany Elachi kutoka kundi la Heaps Up Alliance amesema sasa ni wakati wa kuwasaidia watoto kupanga namna ya kutumia muda ambao ulikuwa unamalizwa kwenye mitandao ya kijamii. Ingawa alikosoa serikali kwa kuchelewa kutangaza majukwaa yatakayohusika, amesema kanuni ya kuwalinda watoto chini ya miaka 16 ni hatua sahihi.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.