MTANGAZAJI

MARUFUKU YA MITANDAO YA KIJAMII NCHINI DENMARK

Serikali ya Denmark imetangaza mpango mpya wa kupiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya miaka 15, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na ongezeko la hatari za kimtandao kwa watoto. Hatua hii imekuja wakati ambapo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 94 ya watoto chini ya miaka 13 nchini humo tayari wanamiliki akaunti kwenye angalau jukwaa moja la mitandao ya kijamii.

Waziri wa masuala ya Kidijitali, Caroline Stage, amesema watoto wanapata muda mwingi mtandaoni na kukutana na maudhui ya vurugu na kujidhuru, jambo analosema ni hatari kubwa kwa ustawi wa watoto. Serikali imeeleza kuwa marufuku hiyo haitaanza mara moja, kwani bunge linatarajiwa kuchukua miezi kadhaa kupitisha sheria husika.

Mpango huo unatoa nafasi maalum kwa baadhi ya wazazi kuruhusu watoto wao kutumia mitandao ya kijamii kuanzia umri wa miaka 13, endapo watapitia tathmini ya kibinafsi. Serikali ya Denmark pia inapanga kuanzisha programu ya uthibitishaji wa umri ili kuhakikisha utekelezaji wa marufuku hiyo.

Hatua hii imekuja kufuatia mfano wa Australia, ambayo tayari imepitisha sheria inayokataza watoto chini ya miaka 16 kumiliki akaunti za mitandao ya kijamii, hatua ambayo majukwaa makubwa kama TikTok, Facebook, Snapchat na Instagram yanakabiliwa na faini kubwa endapo yatakiuka.

Wizara ya Kidijitali ya Denmark imesisitiza kuwa hatua hii sio kupiga marufuku teknolojia kwa watoto, bali kuhakikisha wanaepushwa na maudhui hatari mtandaoni. Ikumbukwe kuwa, Umoja wa Ulaya kupitia Sheria ya Huduma za Kidijitali tayari unakataza watoto chini ya miaka 13 kumiliki akaunti za mitandao ya kijamii.

Katika hatua nyingine, kampuni ya TikTok na Meta zimeeleza utayari wao kushirikiana, huku serikali ya Denmark ikieleza kuwa kampuni hizo za teknolojia zimepewa nafasi nyingi za kuboresha usalama wa watoto lakini hazijafanya vya kutosha.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.