MTANGAZAJI

CHINA INAVYONUFAIKA NA RAIA WAKE WALIOSOMA NG'AMBO

 


Katika juhudi za kukuza maendeleo ya kisayansi, kiteknolojia na kiuchumi, Serikali ya China inaendelea kuwapa kipaumbele wasomi wa Kichina waliopata elimu nje ya nchi. Wasomi hawa wanajulikana kwa jina la “haigui”, neno la Kichina linalomaanisha “wanyama wa baharini waliorejea,” likitumika kama tamathali ya semi kuelezea wasomi wanaorejea nyumbani baada ya kusoma ng’ambo.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Blue Paper ya mwaka 2025, iliyotolewa na Kituo cha Huduma kwa Wasomi Waliosoma Nje (CSCSE), jumla ya wahitimu 366,380 walirejea China mwaka 2023, ongezeko la takriban 30,000 kutoka mwaka uliotangulia. Kati ya hao, asilimia 57 walikuwa wanawake, huku asilimia 63.1 walikuwa na shahada ya uzamili. Idadi ya wahitimu wa shahada ya uzamivu (PhD) pia iliongezeka hadi 21,574, ikiwa ni ongezeko la asilimia 51 tangu mwaka 2020. 

Hata hivyo, ni asilimia 36.8 tu ya wahitimu hao waliobobea katika taaluma za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM), ikilinganishwa na asilimia 58 mnamo mwaka 2020.

 Wasomi hawa haigui wanapewa kipaumbele katika nyanja mbalimbali. Serikali ya China huwapa motisha ikiwemo ruzuku za makazi, mishahara ya juu, ufadhili wa utafiti, na fursa za kuongoza miradi ya kitaifa.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 78 ya wakuu wa vyuo vikuu, pamoja na asilimia 72 ya wakurugenzi wa maabara za kitaifa na kimkoa, ni wahitimu waliorejea kutoka nje ya nchi. Aidha, zaidi ya asilimia 40 ya washindi wa Tuzo Kuu za Kitaifa za Sayansi na Teknolojia mwaka 2023 walikuwa ni haigui, wakionyesha mchango wao mkubwa kwa taifa.

Miongoni mwa wasomi waliorejea China na kuleta mabadiliko makubwa nchini humo ni pamoja na Qian Xuesen, mwanasayansi aliyesomea Marekani, ambaye alichangia pakubwa katika maendeleo ya teknolojia ya makombora na nyuklia ya China. Pia kuna Robin Li, mwanzilishi na mkurugenzi wa kampuni ya teknolojia ya mtandaoni Baidu, na Charles Zhang, mwanzilishi wa Sohu, ambaye alisomea Marekani kabla ya kuanzisha mojawapo ya majukwaa makubwa ya habari mtandaoni nchini China.

Kupitia programu za serikali kama "Thousand Talents Plan", China inaendelea kuwahamasisha wasomi wake walioko nje kurudi nyumbani ili kushiriki katika ujenzi wa taifa. Programu hizi hutoa motisha ya kifedha, fursa za kitaaluma, na mazingira bora ya utafiti kwa lengo la kuimarisha ushindani wa kimataifa wa China katika nyanja mbalimbali.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.